Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema wananachi wakitumia vizuri mitandao ya kijamii, wanaweza kupata taarifa za wanaonyanyaswa, kuonewa na kufanyiwa kazi kwa muda muafaka na watetezi mbalimbali nchini.
Pia umesema ni vyema mitandao ya kijamii ikawa ngao kwa kutumika vizuri kutoa taarifa kama ambavyo inafanywa na baadhi ya mitandao bila ya upotoshaji.
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao huo, Onesmo Olengurumwa akiwa katika maadhimisho ya sita ya siku ya watetezi wa haki nchini, alisema kwa mwaka huu wanatarajia kufanya kampeni ya kuwahamasisha watu kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo ya msingi pamoja na kudai Katiba mpya.
Alisema kwa sasa kuna wimbi kubwa la watu wanatumia mitandao ya kijamii kwa mambo yasiyo ya msingi hivyo wataandaa kampeni maalumu ya kuhamasisha watu kutumia mitandao kwa mambo ya msingi ikiwemo la katiba mpya, kujua haki zao pamoja na mambo ya kuzingatia katika chaguzi ya serikali za mitaa.
Aidha alisema licha ya kuhamasisha watu kutumia mitandao ya kijamii kwa mambo ya msingi pia wataanzisha kampeni maalumu.
Olengurumwa pia alisema wameiomba serikali kwa mwaka huu wahakikishe wanakuwa na sheria ya kuzilinda data za mitandaoni ili kuwa huru katika kuchangia mazuri na hata kukosoa bila kuvunja sheria za nchi.
Alisema wanaomba kupata sheria hiyo ambayo italinda data zote za mitandao ya kijamii na zile ambazo zinatoka sehemu mbalimbali kwenda kwenye mitandao hiyo ya kijamii kwa lengo la kudhibiti waharibifu wa kimtandao.
“Afrika kuna watu milioni 400 kati ya bilioni 1.3 wapo katika mitandao ya kijamii, duniani watu bilioni nne wapo mitandaoni hapa kwetu Tanzania tupo watu milioni 25 wapo mitandaoni kwa nini sasa tusilinde data hizi na kuhamasisha watu watumie mitandao kutetea haki za binadamu,”alisema Olengurumwa.
Alisema watetezi wa haki za binadamu ni kundi kubwa linalojumuisha waandishi wa habari wanaofanya kazi ya kufuchua na kukemea maovu mbalimbali wanayofanyiwa wananchi.
Hata hivyo alisema siku hiyo ya watetezi hapa nchini ni maalumu kwa kutafakari juu ya kazi pamoja na kuwatambua watetezi wote wa haki za binadamu waliofanya kazi kubwa iliyosababisha hata kuumia wakati wakitetea haki za watu wengine.
“Agenda kubwa ya mwaka huu ni kulinda nafasi za watetezi katika mitandao ya kijamii na mtakubaliana na mimi kuwa maisha ya watu wengi sasa hivi yapo mitandaoni, mitandao hii imekuwa ni chombo kinachosaidia haki ieleweke, ilindwe hivyo duniani kote tunatambua kuwa mitandao ndio maisha, “alisema.
Maria Sarungi ni mmoja kati ya watetezi wa haki za binadamu aliyepata tuzo kwa mwaka huu aliitaka serikali kuacha kubughuzi kundi kubwa la vijana linalotumia mtandao katika kutetea na kudai haki mbalimbali .
Alisema si kila kinachoandikwa na vijana cha kudai haki mtandaoni kikawa ni cha kupingwa na hata kusababisha kukamatwa, hivyo ni jukumu la serikali na wahusika wa mtandao katika kuwaelimisha na si kuwakamata.
“Kama mimi nikiwa kama mwanamke wakati mwingine napata matusi mitandaoni watu wanatumia hata jina langu na kutukana watu hivyo ni jukumu la wahusika kukemea hili pia,”alisema Sarungi.
Alisema kitu chochote ambacho watetezi wa haki za binadamu wakiposti katika mitandao ya kijamii uonekana ni uchochezi jambo ambalo si kweli kwani mambo hayo yanalenga kuelimisha.
Naye mwakilishi kutoka Foundation for civil Society (FCS), Sarah Masenga alisema wao wapo pamoja na watetezi katika kusaidia na kuongeza nguvu na kuwataka wafanye kazi za utetezi.
Mwakilishi kutoka kampuni ya simu TTCl, Janeth Maida alisema kama watoa huduma wa kkimtandaowanafanya kazi na watu wote kwa kuwaunganisha pamoja kwenye mawasiliano.