25.6 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Saa 24 ngumu wananchi mikoa ya kusini

Na FLORENCE SANAWA-MTWARA

WANANCHI wa Mkoa wa Mtwara wamekuwa na saa zaidi ya 24 ngumu tangu juzi Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ilipotoa tahadhari juu ya kimbunga Kenneth kupiga mikoa ya kusini.

Wengi wameonekana kuanza kuhama makazi yao wakitembea kando ya barabara wakielekea maeneo ya Majengo, Tandika, Mang’amba, Naliendele na Uwanja wa Ndege waliyoelekezwa kwa ajili ya tahadhari.

Hata hivyo baadhi wameonekana wakipuuzia taarifa hizo na kuendelea kukaa kwenye makazi yao. 

 Wengi walioonekana kuitikia wito wa kuondoka maeneo hatarishi yakiwamo yale ya mabondeni na yaliyo kando ya bahari ni wanawake na watoto.

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda, alisema baadhi ya wananchi wameonekana kukaidi agizo la kuchukua tahadhari jambo ambalo linaweza kuwaletea madhara.

“Wapo hawaamini hizi taarifa za uwepo wa kimbunga,  wanapaswa wajue kikitokea sio kama Mubarak ya kawaida, kina msukumo mkubwa na kina athari kwenye majengo, ni vema tahadhari ikachukuliwa.

“Yapo maeneo mengi tuliyotenga, baadhi ya wananchi wameitikia, lakini tunaamini wapo wazee na wagonjwa tunajitahidi ili waweze kufika katika maeneo hayo kutokana na umbali uliopo,” alisema Mmanda.

Naye Moza Kazumali, mkazi wa Magomeni, Mtwara Mikindani aliyekimbilia Shule ya Msingi Majengo, alisema watu wanapaswa kuacha kudharau maagizo ya wataalamu. 

Alisema kuchukua tahadhari kunaweza kuwasaidia watu wengi kutoka katika majanga.

“Lazima uwe na wasiwasi, tunaona nchi zingine hali inavyokuwa mbaya wanapopata majanga ya uwepo wa kimbunga, tumeona viongozi wetu wametutahadharisha lazima tuwe makini, ubishi sio mzuri,” alisema Kazumali.

Michael Onesmo, mkazi wa Chuno, Manispaa ya Mtwara Mikindani, alisema kufuatia taarifa hizo amelazimika kuhama kwa muda ili kuweza kujinusuru na janga la kimbunga hicho. 

“Sisi kwakweli tumefunga nyumba, hatuwezi kusikia taarifa za wataalamu tukazipuuzia, hata viongozi nao wametusihi,” alisema Onesmo.

Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Mtwara, Christina Sunga, alisema wananchi wanapaswa kukusanyika maeneo yaliyotengwa ili kutoa huduma kwa urahisi. 

“Lengo la kuwakusanya wananchi inakuwa rahisi kuwasaidia tofauti na kuwaacha kila mmoja akiishi kwake.

“Kila mwananchi akiwa kwake ni ngumu kuwasaidia, Serikali haitaweza kumsaidia kila mmoja nyumbani kwake endapo maji yatakuwa mengi, wananchi wanapaswa kutembea pembezoni mwa nyumba ili kuwanusuru na majanga ya maji,” alisema Sunga.

Meneja wa Hali ya Hewa Kanda ya Kusini, Daud Amas, alisema kimbunga hicho hakitakuwa na madhara makubwa kwa kuwa kitatokea bahari kuu. 

“Kimbunga kinapita bahari kubwa kuelekea nchini Msumbiji, kitakuwa na madhara, lakini sio makubwa sana, kimbunga kitapita pembeni sio katikati, wananchi wasiwe na hofu sana,”  alisema Amas.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles