JUBA, SUDAN KUSINI
RAIS wa Sudan Kusini, Salva Kiir amejitolea kuwa mpatanishi katika kuidhinisha mageuzi ya kisiasa nchini Sudan baada ya kupinduliwa kwa Rais Omar al-Bashir, Shirika la Habari la Reuters linaripoti.
Hatua hii inajiri miezi saba baada ya Bashir kusaidia upatanishi uliowezesha kufikiwa makubaliano ya amani kati ya Rais Kiir na waasi.
“Rais amejitolea kuwa mpatanishi katika majadiliano ya makundi tofauti nchini Sudan kwa matumaini kwamba mageuzi mapya yataidhinisha siku mpya Sudan,” Reuters imenukuu taarifa ya ofisi ya rais.
Mataifa hayo mawili yana historia ndefu na huenda ndiyo sababu Sudan Kusini inaona ina wajibu wa kuhusika katika yanayoshuhudiwa hivi sasa kwa majirani zao Sudan.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 na miaka miwili baada ya hatua hiyo kubwa, taifa hilo changa lilitumbukia katika vita ya kiraia iliyoua watu 400,000 na wengine milioni kukosa makazi.
Rais Kiir na aliyekuwa makamu wake, Riek Machar walitia saini makubaliano ya amani hivi karibuni kumaliza mzozo huo wa miaka mitano.
Mwisho