Na Costancia Mutahaba
ELIMU ni haki ya kila mtoto. Wazazi wanapaswa kuwasomesha sawa watoto wao, iwe wa kike au wa kiume.
Watoto wanapofundishwa darasani, kile wanachofundishwa ‘huishi’ kichwani kwa wote, iwe msichana au mvulana. Kuwasomesha ni msaada mkubwa kwao bila kujali jinsi zao.
Hata hivyo, jamii nyingi za Kiafrika, Tanzania ikiwamo, zimekuwa zikiwabagua watoto wa kike wakiwaona kwamba hawana umuhimu wa kusomeshwa na hivyo kuwaandaa kwa ajili ya kuolewa.
Amekuwa akikosa fursa ya kuipata elimu kutokana na sababu mbalimbali, kubwa ikitajwa kuwa ni mila na desturi, pamoja na umasikini ambao huchangia kwa kiasi kikubwa.
Hapa nchini, mifano ya watoto kukosa elimu kwa sababu ya umasikini au mila potofu ni mingi, ambayo serikali na taasisi mbalimbali zimekuwa zikihakikisha inapambana hatimaye kuwakomboa watoto hao.
Miongoni mwa taasisi zinazojishughulisha na masuala ya kumkomboa mtoto wa kike ni Binti Leo, ambayo imekuwa ikiandaa makongamano mbalimbali kwa ajili ya kuwaelimisha wanawake kutambua haki zao na hata kujua umuhimu wa wao kupata elimu.
Pamoja na mambo mengine, Binti Leo inayoongozwa na Mwenyekiti Agnes Lukanga, imekuwa ikipambana kuhakikisha mtoto wa kike anainuka na kuonesha tabasamu la ushindi kwa jamii.
Binti Leo imekuwa ikipingana na wale wanaodhani kuwa watoto wa kike kazi yao hapa duniani ni kuwa walezi wa watoto na watumishi wa jikoni, na badala yake kuwasisitiza kutambua haki zao za msingi ikiwamo kupata elimu na baadaye kuwa na maisha bora kama ilivyo kwa wanaume.
Ukweli ni kwamba, bila mtoto wa kike kusoma, ni vigumu kwa nchi yoyote ile kusonga mbele kimaendeleo, hii ni kwa sababu maendeleo yote makubwa hutegemea uimara wa mwanamke.
Hivyo basi, kama inavyoaminika kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, basi suala hili litiliwe mkazo kwa wote na si kwa wanaume tu, ambao ndio wanaonekana kuwa bora kuliko watu wengine.
Jamii nchini ifanye kila linalowezekana kuhakikisha kuwa watoto wote wanapata elimu sawa, iwe wa kiume, wakike au hata walemavu ambao nao wamekuwa wakifungiwa ndani na kunyimwa fursa ya kufuta ujinga.