MSANII wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, amesema kuwa lugha ya Kiingereza ni lazima kwa msanii anayetaka kuwa wa kimataifa.
Diamond alipokuwa kwenye mahafali ya darasa la saba Shule ya Rightway, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, alisema
lugha hiyo ilimpa hofu wakati alipokuwa akitaka kufikia soko la kimataifa.
“Mwaka jana nilipata mwaliko wa kutumbuiza kwenye jumba la Big Brother, Babu Tale, akaniambia baada ya onyesho nitafanyiwa mahojiano kwa lugha ya Kiingereza hapo niliingiwa na woga lakini nashukuru sikuulizwa
maswali yaliyohitaji maelezo mengi hivyo nilijibu kirahisi,” alieleza Diamond.
Aliongeza kwamba aliporudi nchini ndipo alipoanza kujifunza lugha hiyo kwa bidii kubwa hadi ameweza kwa
kiasi cha kuweza kuitumia anapokuwa katika mialiko mbalimbali ya kimataifa.
“Nawasihi nanyi mjifunze vitu vingi msivyovijua ambavyo vitakuja kuwapa mafanikio au kuwasaidia siku za mbele,’’ alimaliza.