26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yajitosa rasmi mtoto aliyefungwa maisha jela

ANDREW MSECHU-Dar es Salaam

KAMISHNA wa Idara ya Ustawi wa Jamii katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Naftali Ng’ondi, amesema wanaendelea kufuatilia taarifa za kijana Baraka Nkoko (21) aliyefungwa jela maisha ili kuangalia namna ya kufuata utaratibu wa kisheria katika suala lake.

Nkoko alihukumiwa kifungo cha maisha jela Februari mwaka huu, baada ya kutiwa hatiani na wenzake saba, kwa kosa la kuchoma moto Kituo cha Polisi Bunju, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam Julai 2015.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana, Dk. Ng’ondi alisema tayari ameshaagiza wanasheria kufuatilia kwa undani mwenendo wa kukamatwa kwake na mwenendo wa mahakamani hadi hukumu ili kuona namna ya kuchukua hatua.

“Kama mlivyoona, huyu kijana alihukumiwa Februari mwaka huu. Kabla ya kuhukumiwa alikamatwa na kukaa mahabusu kwa karibu miaka minne, lakini inaonesha alipokuwa akikamatwa alikuwa na miaka 17, kwa maana hiyo alikuwa mtoto. Haya ni mazingira ya kuangaliwa upya katika suala hili,” alisema.

Dk. Ng’ondi alisema kwa sasa tayari wameshapata maagizo kutoka wizarani na wameshaagiza wanasheria kulifanyia kazi kwa kuomba nyaraka za kesi na hukumu na kufanya mapitio ya maeneo ambayo haki ilikiukwa.

Alisema hatua nyingine zinaendelea kwa sasa na wataendelea kufuatilia kujua hatima ya kijana huyo, kwa kuwa ni suala lililoko wazi kwa sasa, kutokana na uwepo wa nyaraka zinazoonesha umri wake.

Ofisa Ustawi wa Jamii Kata ya Bunju, Michael Mihayo, alisema jana kuwa wamepata maagizo kutoka uongozi wa juu na tayari wamewasilisha ripoti ya upande wao kwa Kamishna wa Ustawi wa Jamii.

“Tayari tumeshawasilisha maelezo yetu kwa kamishna. Tunaendelea na taratibu nyingine za kiofisi kwa kadiri tunavyoelekezwa na wakuu wetu,” alisema.

Jumatatu wiki hii, Mihayo aliliambia gazeti hili kuwa Ofisi ya Ustawi wa Jamii iliamua kuchukua hatua baada ya kubaini Baraka alikamatwa akiwa na umri chini ya miaka 18, lakini alijumuishwa na watu wazima kinyume cha sheria.

Mihayo alisema katika hatua za awali, walibaini hata ndugu zake ambao hawakuwapo Dar es Salaam hawakujua nini cha kufanya katika kufuatilia suala lake hadi hukumu ilipotolewa.

Alisema baada ya kuamua kufuatilia, walibaini Baraka alizaliwa Januari 24, 1997 na hadi anakamatwa alikuwa ameishi katika eneo hilo la Bunju kwa wiki moja, kisha kuingia katika mikono ya polisi kupitia msako uliofanywa alfajiri Julai 11, 2015.

Mihayo alisema baada ya hukumu hiyo kutolewa ndipo walipopata vizuri taarifa zinazomhusu kijana huyo, kisha kufuatilia taarifa zake na kubaini kuwa ndugu zake wako Kigoma.

Alisema walipoomba nyaraka za kuzaliwa wake, ikiwemo kadi ya kliniki na cheti cha kuzaliwa, walibaini kulikuwa na tatizo katika mawasiliano na utetezi tangu kukamatwa kwake.

Mihayo alisema baada ya kupata nyaraka hizo, ambazo tayari wanazo, wamejiridhisha kuwa Baraka alikuwa mtoto kwa kuwa alikamatwa akiwa chini ya umri wa miaka 18.

Alisema wanadhani polisi walitumia vibaya mamlaka yao na inaonekana walitumia hasira.

Mihayo alisema pamoja na kosa hilo, walibaini kuwa katika mwenendo wa mashtaka, hakuna mtu aliyetoa ushahidi wa kuthibitisha kushuhudia ushiriki wake katika tukio hilo, kwa kuwa wakati tukio hilo likitokea alikuwa akiuza duka ikiwa ni wiki moja tu tangu alipokabidhiwa kazi hiyo kwa ajili ya kumsaidia kujikimu.

Kaka wa kijana huyo, Yoshua Selemani alisema pamoja na ugumu waliokutana nao tangu kijana huyo alipokamatwa, walilazimika kuendelea na mawasiliano wakiwa Kasulu, Kigoma, suala ambalo liliwawia vigumu kupata taarifa za mwenendo mzima wa kesi hiyo.

Alisema ugumu huo ulitokana na ukweli kwamba hawakuweza kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kijana huyo kutokana na hali ngumu ya kiuchumi waliyonayo, kwa kuwa wanategemea kilimo cha jembe la mkono kuendesha maisha yao.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa Februari 22, mwaka huu, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliwatia hatiani washtakiwa wanane katika shtaka la sita la kuchoma moto Kituo cha Polisi Bunju.

Waliohukumiwa ni Yusuph Sugu (40), Juma Kozo (32), Rashid Liwima (29), Nkoko, Abuu Issa (36), Abraham Mninga (23), Veronica Ephraem (32) na Ramadhan Said (22).

Walikuwa wanakabiliwa na makosa sita likiwamo la kuchoma moto kituo hicho Julai 10, 2015, ambacho ni mali ya umma jambo ambalo ni kosa la kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles