Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM
VIJANA wa Chama cha ACT-Wazalendo wanatarajia kufanya maandamano kesho jijini Dodoma kushinikiza Bunge kufuta azimio lake la kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa vijana wa chama hicho, Karama Kaila alisema lengo la maandamano hayo ni kulitaka Bunge kufuta azimio hilo na kuendelea kufanya kazi na CAG.
“Sababu nyingine ni kulitaka Bunge kuweka kwenye shughuli za Bunge (Order Paper) upokeaji wa taarifa ya CAG ikiwa na saini ya Profesa Assad ifikapo Aprili 10 mwaka huu saa tatu asubuhi.
“Tumefikia uamuzi huu baada ya kujiridhisha kwamba uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai na Bunge kwa ujumla wake kusitisha kufanya kazi na CAG ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeanzisha mamlaka ya CAG na kuzuia kabisa kuingiliwa katika majukumu yake. Hivyo ni wajibu wa kila raia kulinda Katiba.
“Maandamano yataanzia eneo la Nyerere Square jijini Dodoma kupitia barabara ya Jamatini na kuingia barabara ya Bunge hadi Jengo la Bunge jijini Dodoma. Tumemwomba Spika wa Bunge au Naibu Spika wapokee maandamano yetu haya ya amani,”alisema Kaila.
Alipoulizwa endapo wameruhusiwa kufanya maandamano hayo na polisi, alisema “Kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Polisi (police ordinance) ambayo inataka kutoa taarifa saa 48 kabla ya muda wa maandamano, umma ufahamu kuwa tayari tumetoa taarifa kwa OCD-Dodoma,”.
Aliwaomba bila kujali itikadi za vyama kusimama imara kuilinda misingi ya Katiba kwa kujitokeza kwa wingi kwenye maandamano hayo ya amani.
“Kauli mbiu ya maandmaano haya ni NASIMAMA NA CAG au kwa kiingereza #IStandWithCAG.
“Kila mtu mwenye uwezo ama avae fulana yenye ujumbe huo au abebe bango lenye ujumbe huo. Hatutaruhusu mabango yenye matusi wala kejeli kwa viongozi. Pia hatutaruhusu sare za vyama vya siasa. Ulinzi wa Katiba ya nchi yetu ni wajibu wetu,”alisema.
Vilevile alisema katika maandamano hayo mabaraza ya vijana wa vyama vya NCCR-Mageuzi, Chauma, UPDP na vyama vingine vitatu vitaungana nasi baada ya maamuzi ya vikao vyao vya ndani.
MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, alisema hana taarifa za maandamano hayo.
“Sina taarifa za maandano, nami nakusikia wewe,” alijibu kwa kifupi Kamanda Muroto.
Machi 25, mwaka huu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, aliliagiza Jeshi la Polisi nchini kutoruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Alitoa agizo hilo akiwa Visiwani Zanzibar, ambapo alisema kuna baadhi ya vyama vya siasa vinafanya mikutano ya hadhara, mikusanyiko ya siasa jambo ambalo ni kinyume na utaratibu.
Lugola alisema huu si wakati wa vyama vya siasa kufanya mikutano ya kutambulisha vyama vyao na kunadi sera zao badala yake wajikite katika shughuli za maendeleo.
Alisema kufanya mikutano ya hadhara ni kurejesha nyuma shughuli za maendeleo ambazo wanatakiwa kufanya wananchi ili kujiiingizia kipato na kuimarisha uchumi wa nchi.
Aprili 2 mwaka huu Bunge lilipitisha azimio la kutofanya kazi na CAG, Profesa Mussa Assad kwa kile kilichoeleza kuwa ameudhalilisha mhimili huo.
Akisoma ripoti ya kamati hiyo bungeni, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge hiyo, Emmanuel Mwakasaka alisema kamati yake imemtia hatiani Profesa Assad kwa kuvunja kifungu cha 26 E cha Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Alisema Profesa Assad wakati wa mahojiano na kamati hiyo alionyesha dharau na hakuonyesha kujutia maneno yake.
Alisema bila kupima athari yake alizungumza katika redio ya kimataifa na huko ni kukosa uwajibikaji wa pamoja ni tabia mbaya.
“CAG ni mteule wa Rais na kutokana na kuonyesha dharau katika kamati, hakuomba msamaha wala kujutia, Bunge haliko tayari kufanya kazi na CAG na haliko tayari kushirikiana naye kutokana na majukumu yake,”alisema.
Wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Profesa Assad alisema Bunge ni dhaifu kutokana na kushindwa kuiwajibisha Serikali pale inapoonekana kuna ubadhirifu.
Kutokana na kauli hiyo CAG alihojiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ambayo ilipendekeza Bunge lisifanye naye kazi na hoja hiyo kupita.
Pia, kamati hiyo iliazimia Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge kutokana na kuunga mkono kauli ya Profesa Assad.