26.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Magufuli: Sijachoka kubadilisha mawaziri

Na ELIZABETH HOMBO

-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amesema hatachoka kubadilisha mawaziri na kwamba wanaopata nafasi hiyo katika uongozi wake wanapitia mateso, kwa sababu hawajui kesho itakuwaje.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Mbinga-Mbamba Bay yenye urefu wa kilomita 66 katika Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Akitolea mfano  Wizara ya Kilimo, Rais Magufuli alisema tayari amebadilisha mawaziri watatu katika wizara hiyo na kwamba anamshukuru aliyepo sasa, Japhet Hasunga anajitahidi kuongoza.

“Nimekuwa kila mara nabadilisha waziri wa kilimo mpaka sasa nimebadilisha kama mara tatu au nne na bado sijachoka kubadilisha, ninamshukuru aliyepo sasa anajitahidi na amesema hapa kuwa mnada wa kahawa unaweza kufanyika hapa Mbinga ili wananchi wapate bei nzuri.

“Lengo ni ili wananchi wasidhulumiwe na hawa matapeli, maana tukiwaendekeza hawa matapeli watahamia kwenye bei ya mahindi mwishowe watahamia kwenye nyumba zetu wavunje na ndoa zetu.

 “Ndugu zangu tunataka Tanzania iwe mahali salama nataka wanunuzi wa kahawa kutoka sehemu mbalimbali duniani waje hapa Mbinga kununua kahawa,”alisema Rais Magufuli.

Aliwataka Watanzania kuwaombea mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi kwa sababu nafasi ya uongozi katika utawala wake ni mateso.

“Kupata uwaziri katika kipindi changu ni mateso kwanza ukiupata huna uhakika kama utamaliza nao, enzi zetu tukiwa mawaziri ulikuwa mpaka mwaka utaisha lakini hawa wana wasiwasi hata wakuu wa mikoa na wilaya.

“Muwaombee kazi hizi ni ngumu kwa sababu hujui kesho litatokea nini ndiyo maana nikasema wanapoteuliwa wasifanye sherehe, maana unaweza ukafanya sherehe kesho jina lako limeshatolewa na kupewa mwingine, nashukuru hawajaniangusha sana na wote ambao bado wako madarakani wanajitahidi sana,”alisema Rais Magufuli.

Alimtaka Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda, vyombo wa usalama na viongozi wengine kuwafichua watu waliofilisi benki ya wakulima wa kahawa ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Waliofilisi benki ya wakulima wa kahawa wako wapi? Ninauliza na nimewahi kuuliza ili mbunge asije akaniuliza mimi kwa sababu matatizo mengine ambayo yanastahili wayatatue huwa hawatatui mpaka rais aje sasa jukumu nimekuachia mbunge kwanini benki ya wakulima wa kahawa imefilisika mpaka leo haipo nani aliyeifilisi na vyombo vya usalama vipo?

“Ninazungumza haya ili tuupate mzizi wa fitna tukiwa tunafunikafunika mambo hatutafika. Viongozi wote kuanzia DC, Takururu, OCD, RPC na RC tuanze kushughulikia hili. 

“Mbunge (Sixtus Mapunda), amezungumza hapa ameeleza kero za wakulima wamelima kahawa yao wamehangaika kwa mwaka mzima, wameweka mbolea wamechuma, wamekausha wamehangaika katika maisha ya kimasikini, wamejitolea kwa ajili ya maisha yao.

“Nafahamu kuna madaraja ya kuuza bei ya kahawa na haiwezi kufanana, kama kahawa ni bei hiyo halafu mwingine apewe bei ya chini mwingine ya juu, hapo lazima tujiulize. Sasa nilitegemea mbunge angeniambia kwamba waliohusika kudhulumu wananchi ni fulani na fulani lakini na yeye ananifichaficha anataka mimi nifuatilie  wakati na yeye alikuwa hapa.

“Ananiambia mimi niliye Dar es Salaam au Dodoma sasa unataka nifanyeje?  Ifike mahali tuache kuogopa na tuache unafiki wataje kwa majina…ungenikabidhi majina hapa ungeona kama wangepumua vizuri leo lakini unayafumbafumba haya maana yake hutaki kupata dawa sasa nataka majina yapatikane.

“Vinginevyo msimu ujao watadhulumiwa hivyo hivyo, sasa inashangaza waliodhulumiwa kahawa zao wako hapa, viongozi nao wako hapa, sasa nataka tuyakomeshe…mshirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama hao watu wapatikane,”alisema.

Alieleza kushangazwa kwa hatua ya viongozi waliopewa mamlaka ya kufanya kazi katika sekta mbalimbali kuwa wabinafsi badala ya kuwatetea wanyonge lakini badala yake wao wamekuwa wanyonyaji.

Akizungumzia kuhusu mradi huo barabara ambao utagharimu Sh bilioni 134.712, alisema mkandarasi alitaka akamilishe mwaka 2021 na kwamba amemweleza kuwa akamilishe mwaka 2020 kwa kuwa fedha zote zipo.

“ Mkandarasi alikuwa amalize barabara hii mwaka 2021 sasa tumemwambia hapana na mimi nataka nifungue  mwaka 2020 hivyo nimemweleza kwa kuwa hela zote  zipo kwanini iwe mpaka 2021? Na wananchi wa kufanya kazi wapo na magereza wapo hivyo nimemwambia wafanye kazi usiku na mchana ili barabara iishie kabla ya 2020,”alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,631FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles