Bunge la Marekani limepiga kura ya kusimamisha ushiriki wa nchi hiyo kwenye vita vya Yemen.
Wabunge 247 walipiga kura kuunga mkono na wabunge 175 waliopinga hatua hiyo ya kusimamisha msaada wa kijeshi unaotolewa na Marekani kwa Saudi Arabia katika vita vya Yemen.
Muswada huo sasa umepelekwa kwa Rais Donald Trump anayetarajiwa kuupinga kwa kutumia kura ya turufu.
Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje wa chama cha Democratic, Eliot Engel amesema Rais Trump anapaswa kukabiliana na ukweli kwamba bunge halitapuuza majukumu yake ya kikatiba kuhusiana na sera za mambo ya nje na kuongeza kuwa vita hivyo vimechangia pakubwa kusababisha mzozo wa kibinaadamu nchini Yemen.
Umoja wa Mataifa umeviita vita hivyo vilivyoingia mwaka wa tano na kusababisha vifo vya maelfu ya raia kuwa ni mgogoro mbaya zaidi wa kibinaadamu kuwahi kutokea duniani.