Ufaransa na Ujerumani zimekubaliana kuanzisha Muungano wa kukuza ushirikiano wa kimataifa katika wakati huu ambapo kuna ongezeko la siasa kali za kizalendo barani Ulaya, Marekani na kwingineko.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Kigeni wa Ujerumani Heiko Maas na mwenzake wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian wamesema katika kikao cha pamoja cha waandishi wa habari kuwa mpango huo utazinduliwa rasmi Seotemba katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Le Drian amesema wamezungumza na Canada na Japan kuhusu mpango huo.
Australia, India, Indonesia na Mexico huenda pia zikajiunga kwenye muungano huo. Lengo la kwanza la muungano huo litakuwa kuonyesha kuwa nchi ambazo zinaunga mkono ushirika wa kimataifa na kuunga mkono Umoja wa Mataifa ndizo zilizo nyingi duniani.