33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CAG Asad: Nahofia mgogoro wa kikatiba

ANDREW MSECHU NA RAMADHAN HASSAN-DAR ES SALAAM/DODOMA

SIKU moja baada ya Bunge kuazimia kutofanya kazi na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, msomi huyo amesema kilichofanywa na chombo hicho cha kutunga sheria kinaweza kuzaa mgogoro wa kikatiba, kwa sababu ripoti yake inatakiwa kuwasilishwa bungeni na Rais kwa ajili ya kujadiliwa.

Akizungumza katika mahojiano na kituo cha Televisheni cha TBC 1 jana, Profesa Assad alisema kinachoonekana kwa sasa huenda kikazaa tatizo kubwa zaidi, hivyo inahitajika busara zaidi katika kuliangalia suala hilo.

“Mimi nafikiri tukae chini tutazame halafu tuone athari ni zipi ili kuepuka tatizo ambalo linaweza kutokea. Ninaamini kuna watu wana busara na ‘probably’ wanatoa busara zao, wasiwasi wangu ni kwamba linaweza kuwa tatizo kubwa kuliko lilivyo sasa hivi,” alisema.

Alipoulizwa kwanini anadhani linaweza kuwa tatizo kubwa zaidi, alisema: “Technically inaweza kuibua ‘constitutional crisis’ (mgogoro wa kikatiba) kwa sababu ripoti (Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2017/18) imeshawasilishwa kwa Rais na mimi siwasilishi ripoti bungeni.

“Kwa hiyo Rais atasababisha ripoti zile ziende bungeni katika siku sita zijazo na kama Bunge litakataa kuzipokea hiyo itakuwa tatizo kubwa zaidi. Kwahiyo wasiwasi wangu ni huo. Na zikishawasilishwa bungeni zinakuwa ‘public document’, mimi ninapata fursa ya kuzungumza.”

Kwa kawaida ripoti za CAG zikishawasilishwa bungeni, yeye hupata fursa ya kuzungumza na vyombo vya habari akiwa na kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kueleza kwa muhutasari kilicho kwenye ripoti hizo.

Kutokana na hilo, Profesa Assad jana alisema; “kwahiyo tafsiri ya kwamba hatutafanya kazi na CAG ni tafsiri pana sana, inatakiwa tuijue vizuri na kama nilivyokwambia mimi bado sijapata hizo habari kwa uhakika (za Bunge kukataa kufanya naye kazi), ninazitafuta leo (jana) na nitaongea na watu wangu, kisha tutafanya tathmini ni nini cha kufanya.”

Alipoulizwa endapo anaweza kuchukua ‘uamuzi mgumu’, Profesa Assad alisema; “Sina maamuzi yoyote ya kuchukua bwana, ninachofanya mimi hapa ni kufanya dua tu basi, watu waongoze vizuri, wafanye maamuzi ambayo yana faida na nchi hii basi, lakini mimi sina cha kufanya, nina ‘constitution duties’ (majukumu ya kikatiba) zangu, nitaendelea nazo na nitaendelea kuzitekeleza.”

Alipoulizwa kuhusu alichoitiwa kwenye Kamati ya Bunge ya Maadili na kama anajutia kauli yake juu ya udhaifu wa Bunge, Profesa Assad alisema; “mazungumzo yote yalifanyika kwenye kamati na yalirekodiwa kwenye ansad, rai yangu tafuta ansad utaona maswali yalikuwa yapi na majibu yalikuwa yapi bwana.”

NDUGAI NA LEMA

Katika hatua nyingine jana Job Ndugai aliagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kukutana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema  (Chadema) ili akathibitishe kama Bunge ni dhaifu kama alivyodai juzi huku akisema wanataka kuthibitisha kwamba Bunge lina uongozi na halimuogopi yeyote.

Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu na kutoa utambulisho wa wageni waliofika bungeni, Ndugai alisema ana tangazo fupi juu ya kilichotokea juzi.

Alisema juzi wakati Lema akichangia juu ya maazimio ya kamati kuhusu kauli ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) kuunga mkono kauli ya CAG kuwa Bunge ni dhaifu, alijilipua kwa kuunga mkono kuwa Bunge ni dhaifu.

“Nadhani wote mnafahamu kilichotokea jana (juzi), Lema alijilipua, kutokana na hali hiyo sasa suala lake naagiza liende kwenye Kamati ya Maadili kama ambavyo Naibu Spika (Dk. Tulia Ackson) alivyoagiza jana na suala lake liishe leoleo.

“Ikiwezekana mambo kesho yawe yamekamilika, kwahiyo Kamati ya Maadili saa nane kamili muanze kikao, saa nane mchana huu, mheshimiwa Lema kuanzia saa saba uwe katika maeneo yale ili uweze kuthibitisha uliyosema jana (juzi), na mimi niwaambie waheshimiwa wabunge Spika Ndugai haogopi.

“Wanaofikiri sisi dhaifu sio dhaifu, nilishasema na kurudia. Yeyote ambaye anataka kuingia kwenye 18 hii, sisi tupo tayari na tutawapeleka huko kwenye kamati ile ambayo baadhi walisema ina udhaifu fulani, basi Lema atakwenda huko, kesho (leo) panapo majaaliwa tutaifahamu hatma yake na mwingine anayejiona yeye anaalikwa kwenye mkutano huo.

“Yani tunataka kuthibitisha Bunge hili la 11 lina uongozi na tutathibitisha kuwa hatumuogopi yeyote,” alisema.

LEMA ANADAIWA

Katika hatua nyingine, Spika Ndugai alisema Lema amekopa Sh milioni 644 na amelipa sh milioni 225 na anadaiwa sh milioni 419.

“Hapa kuna msongo wa mawazo, kwa mfano yapo mambo ambayo hatusemi ila tuseme kidogo. Niwaambie  wananchi mambo mengine hawayaelewi vizuri, ipo misongo mingi ya mawazo humu ndani labda ndiyo inasababisha mambo hayo.

“Mheshimiwa Lema tangu aje hapa bungeni amekopa milioni 644. Useme aaa… useme eeehh… ameishalipa  milioni 225 na  sasa hivi anadaiwa milioni 419, hiyo ni sehemu ya msongo wa mawazo,” alisema Ndugai.

WABUNGE WAPEWA NENO

Aidha Spika Ndugai alisema wabunge ni wawakilishi wa wananchi, hivyo hawatakiwi kuweka mambo yao binafsi katika uwakilishi.

 “Ninyi ni wawakilishi wa wananchi, mnapokuja hapa lazima muwakumbuke wale mnaowawakilisha, unapotanguliza ‘personal interest’ kwamba mimi siogopi, sio wewe, ni walewale unaowawakilisha, wana haki ya wewe kuwawakilisha.

“Wakati mwingine kati ya wewe na wale lazima upime kipaumbele ni nani, ukiweka kipaumbele wewe, kidogo hapo inakuwa sio sawaswa.

PIUS MSEKWA

Akizungumzia suala la CAG, Spika mstaafu Pius Msekwa alisema japokuwa hana uzoefu na suala kama hilo kwa kuwa halikuwahi kutokea katika enzi zake, lakini anaona Bunge lina mamlaka ya kupitisha azimio la aina hiyo.

“Bunge linasema halina imani na mtu aliyeshika nafasi ya CAG, hii maana yake ni kwamaba halina imani na kiongozi aliyeko sasa,” alisema.

Alisema kwa mtazamo wake haileti mgogoro wowote wa kikatiba kwa sababu katika utumishi wa umma, Bunge halimteui CAG, lakini likimkataa kiongozi yeyote ni suala ambalo lina hatua za kufuatwa kulitanzua.

Msekwa alisema Bunge lina mamlaka na uwezo wa kusema halina imani na Waziri Mkuu na hatua inayofuata ni uamuzi wake kujiuzulu na iwapo atang’ang’ania, suala hilo linaachwa kwa mamlaka ya uteuzi na hilo liko wazi kikatiba.

Alisema kwa hatua iliyofikiwa na Bunge hadi sasa, suala hilo linarudi mikononi mwa CAG mwenyewe na kwa mamlaka ya uteuzi ambayo anawajibika kwayo, ambayo ni Rais.

Msekwa alisema aidha CAG anaweza kuamua kuachia nafasi hiyo na iwapo atang’ang’ania, suala hilo linarudishwa kwa mamlaka ya uteuzi ambayo itatakiwa kufuata utaratibu wa kikatiba wa kumwondoa.

Alisema kwa nafasi ya uteuzi wa CAG, kama ilivyo kwa majaji, si rahisi mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi ila kama mamlaka ya uteuzi itaona inalazimika kumwondoa, kuna utaratibu utakaotakiwa ufuatwe ili kuthibitisha makosa yaliyowasilishwa na kutolewa uamuzi na Bunge, kisha kumtoa katika nafasi hiyo.

Msekwa akizungumzia ripoti ya CAG iliyokabidhiwa kwa Rais wiki iliyopita, ambayo inatakiwa iwasilishwe bungeni ndani ya siku saba tangu kukabidhiwa kwake, alisema hatua hiyo ya Bunge haizuii ripoti hiyo kuwasilishwa bungeni.

Alisema Bunge limeonesha kutokuwa na imani na mtu anayeshikilia nafasi ya CAG kama kiongozi wa idara, lakini siyo kutokuwa na imani na idara, hivyo ripoti hiyo inatakiwa iwasilishwe bungeni kama ilivyo ada.

“Anachopeleka Rais bungeni ni ripoti inayotoka kwenye idara. Anapeleka ripoti, hapeleki mtu. Kwahiyo kama iko ndani ya muda ripoti hiyo inatakiwa iwe imeshafika bungeni na itatakiwa kujadiliwa katika utaratibu wa kawaida,” alisema.

ANNA HENGA

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga alisema hatua hiyo ya Bunge ni ya kusikitisha kwa kuwa CAG ndiye mwakilishi wa Serikali katika kuangalia iwapo fedha za umma zinatumika ipasavyo.

Alisema majukumu ya CAG yanawekwa wazi katika Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba atasimamia matumizi ya fedha zote zilizoidhinishwa na Bunge kuhakikisha zinatumika ipasavyo.

“Hatua ya Bunge kukataa kufanya kazi na CAG inaleta maswali mengi sana. Inakiuka na kuvuruga mgawanyo wa madaraka na kukiuka misingi ya utawala bora ambayo inawawajibisha wabunge kuhakikisha wanashirikiana na CAG katika kulinda fedha ya umma,” alisema.

Alisema kwa hatua hiyo, Bunge linakiuka wajibu wake kwa kuvunja mnyororo wa uwajibikaji, hatua inayolifanya lishindwe kutimiza wajibu wake wa kuisimamia Serikali katika matumizi sahihi ya fedha za umma zinazotokana na walipakodi, ambazo zinafanyiwa ukaguzi na CAG.

FATMA KARUME

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Fatma Karume, alisema uamuzi huo wa Bunge ni wa kushangaza kwa sababu suala la Bunge kufanya kazi na CAG si la hiyari, bali ni la lazima kwa mujibu wa katiba.

“Wataacha vipi kufanya kazi na mtu ambaye katiba inawaambia kwamba ni lazima? Katiba inawalazimisha hawa, si suala la hiyari. Tena katiba haiwaambii wafanye kazi na CAG anayewapendeza, wanatakiwa wafanye kazi na yeyote aliyeko kwenye nafasi, aidha anawapendeza au hawapendezi.

“Kama wasipofanya kazi naye wanavunja katiba. Tena kazi yao si kumvuruga CAG ila asilete ripoti au kuvuruga mazingira ili ripoti yake isifikishwe bungeni, hata kama wanaona kuna mambo yao wanayotaka kuyalinda,” alisema.

Alihoji kuwa iwapo hoja ya kauli ya CAG kuwa Bunge ni dhaifu ndiyo iliyowakera wabunge, kama yeye angekuwa mbunge angechukua hatua ya kuipitia ripoti ya CAG vizuri ili aone udhaifu wake naye amuumbue katika hilo.

“Eti unaitwa dhaifu halafu unakataa kushirikiana naye, unakataa kazi yake, siyo kwamba unatoa sababu kuwa kazi yake haiwezi laa. Huwezi kukataa kufanya kazi uliyotumwa na kuelekezwa na katiba kwa sababu za rejareja,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles