WASHINGTON, MAREKANI
MWANASHERIA maalumu Robert Mueller amewasilisha matokeo ya ripoti yake ya siri kuhusu uchunguzi wa nafasi ya Urusi kuingilia uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 nchini Marekani.
Uchunguzi huo ambao umedumu kwa kipindi cha miaka miwili ambao tayari umewanasa washirika wa zamani wa Trump na maafisa wa ujasusi wa Urusi na kuibua maswali kuhusu nafasi ya rais huyo katika wadhifa wake.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times limesema kuwa Mwanasheria Mueller amekabidhi ripoti hiyo kwa Mwanasheria Mkuu William Barr kwa hatua zaidi za kisheria.
Katika uchunguzi wake, Mueller aliwashitaki watu 34 na kampuni tatu kwa kuhusika na suala la uchaguzi wa mwaka 2016.
Swali kubwa sasa ni kama ripoti hiyo ambayo inaibua mjadala wa iwapo Trump alifanya makosa yoyote au kama hatapatikana na makosa yoyote. Miongoni mwa watu hao ni aliyekuwa kiongozi wa kampeni za rais huyo, Paul Manafort na mshauri wake wa kwanza wa usalama wa taifa Michael Flynn.
Wengine ni watu 25 raia wa Urusi walishitakiwa kwa mashitaka yanayohusiana na uingiliaji uchaguzi wakituhumiwa kwa kudukua akaunti za barua pepe za chama cha Democratic wakati wa kampeni au kupanga kampeni ya mitandao ya kijamii ambayo ilisambaza habari za uongo kwenye intaneti.
Wasaidizi watano wa Trump walikiri kuwa na hatia na wakakubaliana kushirikiana na Mueller katika uchunguzi wake.
Trump alikanusha madai kuwa alishirikiana na serikali ya Urusi wakati wa kampeni za urais kwa ajili ya kupata ushindi. Urusi pia inakanusha kuingilia kwa njia yoyote uchaguzi huo
Hatua inayofuata sasa ipo mikononi mwa Mwanasheria Mkuu William Barr, ambaye ana jukumu la kuandika ripoti yake kuhusu matokeo ya uchunguzi wa Mueller na kuituma katika Bunge la Marekani.
Katika barua kwa wabunge, alitangaza kuwa amejitolea kuhakikisha uwazi na kuharakisha mchakato huo. Kwa upande wao Ikulu ya White House imejitenga na ripoti hiyo ikisema haijaiona wala kufahamishwa chochote kuihusu.
Kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ya Mueller kuna maana kuwa uchunguzi umekamilika bila mashtaka yoyote ya umma ya njama ya uhalifu kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi au kizuizi kilichowekwa na rais huyo.
Afisa wa Wizara ya sheria ya Marekani amethibitisha kuwa Mueller hatopendekeza mashtaka mengine zaidi.
Duru za kiaisa ziansema hizo ni habari nzuri kwa washirika kadhaa wa Trump na jamaa zake waliokumbwa na hatia ya kufanya makosa. Waliokuwa na hatia ni Donald Trump Jr., ambaye alikuwa na jukumu la kupanga mkutano na wakili aliyekuwa na mahusiano na serikali ya Urusi, kwenye jengo la Trump Tower wakati wa kampeni za urais 2016.
Mwingine ni mkwe wa Trump, Jared Kushner, ambaye alihojiwa alau mara mbili na waendesha mashitaka wa Mueller.