33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

TAIFA STARS TWENDE KAZI

NA MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo kitashuka dimbani kutafuta ushindi muhimu dhidi ya  Uganda ‘Cranes’, katika mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za mataifa Afrika (Afcon) utakaochezwa Uwanja Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ni karata muhimu kwa Stars  kushinda ,ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu fainali hiyo zitakazofanyika baadae mwaka huu nchini Misri.

Mgeni rasmi katika mchezo huo atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Hata hivyo, Stars itahitaji ushindi katika mchezo huo, huku ikiiombea mabaya Lesotho ifungwe au itoke sare dhidi ya Cape Verde.

Kama hilo litafanikiwa, Tanzania itaungana na Uganda ambayo tayari imeshafuzu fainali hizo.

Lakini Lesotho ikifanikiwa kupata ushindi wowote dhidi ya Cape Verde, itajihakikishia tiketi ya fainali hizo na kuiacha Stars mikono mitupu.

Lesotho pia inaweza kufanikika na athari za matokeo michezo yake miwili na Stars, ambapo katika mchezo wa kwanza Stars ililazimisha sare ya bao 1-1 nyumbani, kabla ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano jijini Maseru.

Stars inamakata nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi L, ikiwa na pointi tano, sawa na Lesotho inayoshika nafasi ya pili,zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

 Uganda inaoongoza kundi hilo, ikiwa pointi 13, Cape Verde inaburuza mkia, ikiwa na pointi nne.

Stars ilizindua kampeni zake kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Lesotho Juni 10 mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kisha ikalazimisha suluhu ugenini dhidi ya Uganda.

Ikaambulia kipigo cha mabao 3-0  ugenini dhidi ya Cape Verde kabla ya kulipa kisasi  nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 Uwanja wa Taifa.

Baada ya kuikandamiza Cape Verde ikasafiri kwenda Lesotho ambako ilidunguliwa bao 1-0 na wenyeji.

Stars itashuka dimbani leo, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kutoka suluhu na Uganda ugenini,  Uwanja wa Nelson Mandela ‘Namboole’, Kampala.

Rekodi  za Stars dhidi ya Uganda

Mchezo huo utakuwa wa 54 kuzikutanisha timu hizo katika mashindano mbalimbali, tangu mwaka 1964, Stars imeshinda michezo sita, huku Uganda ikishinda 26, michezo 12 ikimalizika kwa sare.

Mabao 142 yamefungwa kupitia michezo hiyo, Uganda ikizamisha 90 na Stars mabao 52

Rekodi za michezo mitano ya mwisho ya timu hizo zinaonyesha, Uganda imeshinda miwili na kutoka sare mitatu.

Mara ya mwisho Stars kupata ushindi nyumbani dhidi ya Uganda ilikuwa mwaka 2007, ilishinda bao 1-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki. Bao pekee la Stars lilifungwa na kiungo Abdi Kassim ‘Babi’.

Stars ya 1980

Mara ya mwisho Tanzania ilishiriki Afcon mwaka 1980, fainali hizo zilipofanyika nchini Nigeria.

Toka wakati huo hadi sasa imepita  miaka 39.

Stars ilitinga katika michuano hiyo baada ya kutupa nje Zambia ya ambayo ilikuwa zilizogopwa Afrika.

Mchakato wa kufuzu wakati huo ulikuwa kwa mtindo wa mtoano, ambapo Stars ilianza kwa kumenyana na Mauritius ugenini na kukubali kichapo cha mabao 3-2, kabla ya kupindua matokeo nyumbani na kushinda mabao 3-0, hivyo kusonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 5-3.

Stars ilianza kwa kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Zambia ‘Chipolopolo’, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru , Agosti mwaka 1979, bao hilo lilifungwa na Mohamed Rishard ambaye kwa sasa ni kocha wa timu  Tanzania Prisons.

Katika mchezo wa marudiano uliochezwa mjini Ndola, Stars ilihitaji sare tu ili kufuzu, katika mchezo huo wenyeji walianza kupata bao la mapema, lakini Stars ilisawazisha dakika ya 87 na kufuzu.

Bao la Stars lilifungwa na mshambuliaji, Peter Tino.

Kikosi cha Stars kilikuwa kinanolewa na kocha, Slowmir Work  raia wa Poland, akisaidiwa na wazawa Joel Bendera (marehemu) na Ray Gama.

Kikosi cha Stars kilikuwa kinaundwa na wakali, Athumani Mambosasa(marehemu) ,Juma Pondamali,Taso Mutebezi,Jelah Mtagwa,Leodgar Tenga,Mohamed Kajole (marehemu),Hussein Ngulungu,Mtemi Ramadhan,Juma Mkambi (marehemu),Omari Hussein,Mohamed  Salim,Thuweni Ally na Peter Tino

Wengine ni Salim Amiri,Mohamed Rishard,Thuwen Ally , Rashid Chama ,Charles Alberto, Daud Salum,Ahmed Amasha,Salim Amiri, Idd Pazi.

Mwakyembe anena

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, amekitaka kikosi cha Stars kutumia mbinu zilizotumiwa na  Simba kuifunga  timu ya AS Vita ya DRC na kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuitungua Uganda leo.

“Ni lazima tuwafunge Uganda kwasababu ni timu ya kawaida, cha msingi ni wachezaji wetu kuwa makini uwanjani, mashabiki wajitokeze kwa wingi kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa Simba.

“Ni zamu yetu kwenda Misri, Watanzania tuungane kwa pamoja na kujitokeza kwa wingi ili kuisapoti Taifa Stars,” alisema Mwakyembe.

MAKONDA

Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya Taifa Stars, Paul Makonda ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani na kushangalia kwa nguvu ili kuwapa morali wachezaji.

Makonda ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisema shabki ni mchezaji wa 12, hivyo kujitokeza kwa wingi kutakuwa chachu ya Stars ya kupata ushindi dhidi ya Uganda na kufuzu Afcon.

“Naomba tujitokeze kwa wingi uwanjani, lakini tusifike na kukaa, bali tushangilie kwa nguvu mchezaji wetu anapopata mpira ili asijihisi yuko peke yake, lakini tuzomee pale wapinzani wetu wanapopata mpira ili kuwapa mchecheto na kushindwa kufanya maamuzi sahihi.

“Watanzania tunapaswa kuwa kitu kimoja wakati huu, umoja wetu utakuwa silaha kubwa, kila mmoja wetu analo jukumu ya kuisaidia Stars kushinda, tusiwaachie wachezaji pekee, tuhamasishane ili kufanikishe mpango huu,” alisema Makonda.

Tenga hayuko nyuma

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodagal Tenga amewataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wanapambana kwa nguvu zao zote ili kuhakikisha wanapata ushinda kwenye mchezo.

“ Samatta(Mbwana) unatakiwa kuwaongoza wenzako katika kuhakikisha mnatumia vema faida ya kucheza  nyumbani kujipatia ushindi utawaowawezesha kufuzu.

“Mnatakiwa kupigania taifa, Watanzania wote wako nyuma yenu, hakikisheni mnatumia vema nafasi hii kwenda Afcon, uwezo mnao, ongezeni tu juhudi nina imani kubwa hamtatuangusha.

 “Nakumbuka sisi tulicheza Uwanja wa Uhuru(zamani  Taifa), tulipambana kweli kweli na hata tulivyokwenda ugenini hatukuruhusu kufungwa hadi tukafanikiwa kufuzu, naamini mtaweza kutufikisha huko,” alisema Tenga.

Amunike atema cheche

Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike amesema kikosi chake kimejipanga vizuri kuhakikisha kinatumia vema uwanja wake wa nyumbani kujipatia ushindi na kufuzu Afcon.

Alisema timu hiyo ina nafasi ya kubwa ya kushinda mchezo huo, kwa kuwa itakuwa nyumbani ambapo itapata sapoti ya Watanzania.

“Tumejipanga vizuri kwa mchezo huo, najua ugumu wa mchezo huo na umuhimu wake, tunafahamu Uganda ni timu nzuri, lakini hata sisi pia ni timu bora, tulikutana nao kwao na kutoka nao sare, tuna kila sababu ya kushinda nyumbani ambapo tutacheza mbele ya ndugu na jamaa zetu,” alisema staa huyo wa zamani wa Super Eagles.

Samatta asisitiza

Nahodha wa kikosi hicho, Samatta alisema watahakikisha wanapambana na kuwapa raha Watanzania kwa kupata ushindi katika mchezo huo.

Mshambualijia huyo anayeichezea KRC Genk ya Ubelgiji alisema, wao kama wachezaji wana jukumu la kupambana ili kushinda mechi hiyo ngumu na kumaliza ukame wa kutofuzu Afcon kwa miaka 39.

“Haina jinsi itabidi tupambane ili tuweze kupata ushindi nyumbani na kuandika historia mpya ya kufuzu Afcon kwa mara ya pili,” alisema Samatta.

Msuva  akazia

Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Simon Msuva anayekipiga klabu ya Difaa Hassan El Jadida ya Morocco alisema mipango yao ni kuitoa Tanzania kimasomaso  kwa kupata ushindi.

“Hii ni zamu yetu Tanzania, hivyo tutahakikisha tunapata ushindi nyumbani ili tuweze kupata nafasi ya kushiriki fainali hizo na kuzidi kuweka Tanzania katika ramani nzuri ya soka Afrika,”alisema Msuva.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles