25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Simu gerezani zawaondoa askari magereza wanne

PENDO FUNDISHA-MBEYA

NAIBU Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amemwagiza Kamishna Jenerali wa Magereza, Phaustine Kasike, kuwasimamisha kazi askari wanne wa Gereza la Ruanda jijini Mbeya kwa tuhuma za kukiuka maadili ya kazi.

Ameagiza askari hao wasimamishwe kwa kosa la kushirikiana na wafungwa kuingiza simu na dawa za kulevya gerezani.

Aliwataja askari hao wanaotakiwa kusimamishwa kazi kuwa ni Inspekta Longino Mwemezi, WDR Ramadhan Mhagama, Alexander Mwinjano na Benjamini Malango, ambao wote wana cheo cha Sajentaji wa magereza.

Pia, Masauni ameliagiza Jeshi hilo kuunda kamati itakayochunguza mtandao wote wa uhalifu uliokuwa ukitumika  kwa kutumia simu pamoja na kuingiza dawa hizo za kulevya na kwamba pindi wakibainika wengine nao wachukuliwe hatua za kisheria.

Agizo hilo, amelitoa jana alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo ambapo licha ya Rais kuyataka majeshi mbalimbali kubadili mfumo wa utendaji kazi wao likiwemo jeshi hilo la magereza nchini, bado baadhi ya askari wameendeleza vitendo vya ukiukwaji wa sheria na maadili ya kazi.

Alisema katika uchunguzi wa awali, umefanikisha kukamata simu tisa zilizokuwa zikitumiwa na wafungwa gerezani kwa mawasiliano na mpango huo ulikuwa ukifanywa na baadhi ya askari wa jeshi hilo.

Alisema pia walibaini kuwepo kwa vitendo vya uingizwaji wa dawa za kulevya aina ya bhangi na kuuziwa baadhi ya wafungwa jambo ambalo ni kinyume cha taratibu na kanuni za jeshi ikiwa na sheria mama za nchi.

 “Simu hizi tulizikamata jana katika msako uliokuwa unafanyika ndani ya gereza hili la Ruanda, tulizikabidhi kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa uchunguzi wa awali na kubaini mambo mengi yaliyokuwa yakifanyika ikiwa ni pamoja na baadhi ya watu waliokuwa wakishirikiana na wafungwa hao gerezani,” alisema.

 “Namwagiza pia Kamishna Jenerali wa Magereza kuunda tume ya kuchunguza vitendo hivyo ili kubaini mtandao mzima uliokuwa unahusika na wakibainika wengine hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema Masauni.

Aidha, Naibu Waziri Masauni, aliwataka wakuu wa magereza yote nchini kuwa makini kwa kuzuia vitendo hivyo vya ukiukwaji wa sheria na maadili visifanyike ili kulinda usalama wa maeneo hayo ambayo ni hatarishi.

Masauni baada ya kutembelea gereza hilo la Ruanda na kuzungumza na wafungwa, pia alitembelea gereza la Kilimo la Songwe kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa agizo la Serikali la wafungwa kutumika kwenye uzalishaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles