Na Fredy Azzah-Zanzibar
ZIKIWA zimepita siku tano tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kujiunga ACT Wazalendo na kukabidhiwa kadi namba moja, inaelezwa kadi namba mbili imechukuliwa na kigogo mmoja mkubwa kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye bado hajatangazwa hadharani.
Kwa mujibu wa kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, tangu kuanzishwa kwa chama hicho 2014 hadi sasa, wamegawa zaidi ya kadi 450,000 huku kwa siku tano tangu Maalim Seif kujiunga nao, wameshatoa kadi 15,000 kwa wanachama wapya.
“Hapa tumeishiwa na kadi kabisa, tulizochapisha kwa ajili ya kupokea wageni hawa zimeisha imebidi turudi tena kuchapisha nyingine,” alisema Zitto.
Machi 18, mwaka huu, Maalim Seif, alipojiunga na chama hicho, alipewa kadi namba moja ambayo ilielezwa kuwa awali ilitolewa kwa aliyekuwa Mshauri wa Sheria wa Chama hicho, Albert Msando, ambaye baadaye alijiunga na CCM na kujivua uanachama wa ACT.
Baadhi ya viongozi wa chama hicho, wanasema kadi namba mbili imeshatolewa kwa mmoja wa kigogo wa CCM ambaye pia alipata kuhudumu serikalini na kushika nafasi nyeti wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Mtanzania ilipomtafuta Zitto kujua ukweli wa suala hilo, alisema: “Wapo wanasiasa waandamizi wengi tu ambao wengine waliwahi kuwa viongozi waandamizi wa Serikali ya CCM, wametupigia simu kutupongeza baada ya kuona safari yetu hii na wengine wameonyesha nia ya kujiunga na sisi.
“Sasa atakuwa ni nani, ni mapema kumtaja ama kuwataja, tusubiri muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi na haya mambo ya kuhisi ni fulani ama fulani yataisha,” alisema Zitto.
Mbali na Maalim Seif mwenye kadi namba moja, Zitto alisema mwenye kadi namba mbili atajulikana muda ukifika huku namba tatu akisema ipo kwa Chiku Afah Abwao, namba nne Mansoor Himid, namba tano, Thomas Msasa na namba saba, Sakina Dewji.
Alisema kadi namba nane ni yake mwenyewe Zitto, namba tisa Venance Msebo na namba 10 ni Juma Duni Haji.
Maalim Seif, mwamba wa siasa za Zanzibar, ameanza safari mpya ya kisiasa ndani ya chama cha ACT- Wazalendo, akikabidhiwa kadi namba moja.
KADI YA DARAJA LA JUU
Zitto alisema kadi zilizokabidhiwa kwa Maalim Seif na wenzake zilikuwa za daraja la juu (premium) ambazo nyingi zilinunuliwa na viongozi wakiwamo wale waliohama na kwamba aliyopewa Maalim Seif iliachwa na Msendo.
Alisema kabla ya Maalim kadi hiyo ilinunuliwa na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS), Venance Msebo, ambaye alielekeza apewe mwanasiasa huyo wa muda mrefu.
“Ukiwa kiongozi ambaye upo kwenye mioyo ya wananchi kamwe hawawezi kukutupa,” alisema Zitto.
Zitto alisema Msebo, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya ACT-Wazalendo, amelipa fedha ya kadi shilingi 500 na malipo ya ada ya miaka kumi, kila mwaka ni shilingi 1,000.
Alisema kadi hizo zinatakiwa kukombolewa kwa sababu zilitolewa kwa watu maalumu ambao walikumbwa na dhoruba ya kuhama chama.
Kwa mujibu wa Zitto, wakati chama hicho kinaanzishwa zilitengenezwa kadi kuanzia namba moja hadi 1,000 ambazo ziliuzwa kwa bei kubwa lakini baada ya baadhi kuamua kutimkia CCM kadi hizo zilikombolewa kisha kupewa wanachama hao wapya.
Kadi namba mbili inayodaiwa kuchukuliwa na kigogo huyo wa CCM, awali ilikuwa ikimilikiwa na aliyekuwa Katibu wa ACT- Wazalendo, Richard Mwigamba ambaye naye alitimkia CCM.
Wengine waliokuwa na kadi hizo ni Profesa Kitila Mkumbo ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na sasa amejiunga CCM, hivyo kadi yake kupewa Mansour Yussuf Himid.
Katika hilo, Zitto alisema yeye kadi yake ni namba nane na aliichagua hiyo kama heshima kwa aliyekuwa nahodha wa timu ya Liverpool ya Uingereza, Steven Gerrard.
Zitto pia alisema kadi ya aliyekuwa mkurugenzi wa habari CUF, Salim Bimani, atapelekewa kwa kuwa hakuwepo.
Taarifa hizo za kadi namba mbili kuchukuliwa na kigogo wa CCM zimekuja katika wakati ambao upepo wa kisiasa ukiwa umebadilika ghafla baada ya mkongwe huyo wa siasa za upinzani nchini, Maalim Seif, kujiunga ACT baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kumhalalisha Profesa Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF na kuhitimisha mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka miwili.
Uamuzi huo wa Mahakama ulikuja baada ya Profesa Lipumba kubatilisha uamuzi wake wa kujivua uenyekiti Agosti, 2015 na kurudi madarakani mwaka 2016 hali iliyozua mgogoro mkubwa.
Maalim Seif mwenyewe amekaririwa akisema uamuzi wao wa kujiunga ACT-Wazalendo ni kuendeleza safari ya kudai demokrasia.
Maalim Seif, baada ya kukabidhiwa kadi yake Machi 19, alisema wameshaachana na CUF, ambayo alishiriki kuianzisha mwanzoni mwa miaka ya 1990.
“Tumepeana talaka na CUF na rasmi leo sisi ni wanachama wa ACT- Wazalendo,” alisema Maalim Seif ambaye leo anatarajiwa kuhutubia maelfu ya wafuasi wake kisiwani Pemba.