RIYADH, Saudi Arabia
SERIKALI ya hapa imetangaza kwamba binti Mfalme Rima bint Bandar al-Saud atakuwa balozi wake nchini Marekani, akiwa mwanamke wa kwanza kutoka katika ukoo wa kifalme kushika wadhifa huo.
Uteuzi wake ulifanywa hadharani kwa amri ya ufalme huo juzi na binti huyo mfalme, ambaye alikuwa akiishi mjini Washington DC nchini Marekani katika kipindi kirefu cha utoto wake.
Hata hivyo, binti huyo mfalme anachukua wadhifa huo wakati mgumu, huku Saudia ikijaribu kukabiliana na hisia za jamii ya kimataifa kuhusu mauaji ya mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi.
Baada ya kutoa taarifa zenye utata, ufalme huo baadaye ulikiri kwamba Khashoggi ambaye alikuwa mfanyakazi wa ufalme huo, aliuawa baada ya kuingia ubalozi wa taifa hilo uliopo Istanbul mwaka uliopita.
Kabla ya kifo chake, mwandishi huyo alikuwa akiliandikia gazeti la The Washington Post, ambako mara kwa mara alikuwa akiikosoa Serikali ya Saudia.
Saudia imekana kwamba mwanamfalme Mohammed Bin Salman alihusika katika kifo chake, madai ambayo Idara ya Ujasusi nchini Marekani inatilia shaka.
Hivi majuzi wanachama wa Bunge la Congress walichunguza uhusiano kati ya Saudia na Marekani katika maeneo mengine, ikiwamo kuhusu teknolojia ya kinyuklia pamoja na vita nchini Yemen.
Kwa uteuzi huo, binti huyo atakuwa anafuata nyayo za baba yake, Bandar bin Sultan al-Saud, ambaye alishikilia wadhifa huo wa ubalozi wa Marekani hadi 2005.