JARKATA, INDONESIA
JESHI la Polisi nchini hapa limeomba msamaha kwa kutumia nyoka kumtishia mshukiwa wa wizi baada ya video kusambazwa katika mitandao ya kijamii.
Katika picha hiyo ya video, maofisa hao wa polisi wanaonekana wakicheka, wengine waliokuwa wakimhoji mshukiwa aliyekuwa amefungwa pingu wakimzungusha nyoka shingoni mwake huku akipiga kelele mashariki mwa eneo la Papua.
Inaaminika mshukiwa huyo alikuwa ameiba simu za mkononi.
Akizungumzia tukio hilo, ofisa mkuu wa polisi katika eneo hilo, alisema juzi kwamba haikupaswa kufanyika hivyo, lakini ametetea mbinu hiyo huku akieleza kwamba nyoka huyo hana sumu.
“Tumechukua hatua kali dhidi ya maofisa waliohusika,” alisema ofisa huyo, Tonny Ananda Swadaya na kuongeza kwamba maofisa hao hawakumpiga mshukiwa.
Alisema maofisa hao walichukua hatua kwa hiari yao ili kujaribu kumfanya mshukiwa akiri makosa.
Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu, Veronica Koman ndiye aliyetuma ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter ulioonesha video hiyo, akidai kuwa maofisa hao hivi karibuni pia walimtishia mwanaharakati anayetetea uhuru wa Papua kwa nyoka akiwa gerezani.
Sauti katika mkanda huo wa video inaarifiwa kusikika akitishiwa kumweka nyoka huyo ndani ya mdomo wa mtuhumiwa na ndani ya suruali yake.