Elizabeth Kilindi-Njombe
MKUU wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Venance Mabeyo, ametua mkoani Njombe kufuatilia matukio ya utekaji na mauaji ya watoto yaliyotikisa mkoani humo.
Aamesema Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), litakomesha matukio yote ya mauaji nchini yanayosababishwa na imani potofu.
Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
Alisema baada ya kufikia mkoani hapa amefanya kikao hicho pamoja na vikosi maalumu vilivyopo mkoani hapa kuchunguza matukio hayo.
Jenerali Mabeyo alisema sababu za utekaji na mauaji ya watoto yanahusisha zaidi ngazi ya familia na vyombo vya ulinzi na usalama vimeanza kuchukua hatua kukomesha mauaji hayo.
“Ninapenda kusema kwamba kwa sasa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kwa kushirikiana na jeshi.
“….mimi ndiye mwenyekiti wa vyombo vyote vya ulinzi hivyo ninao wajibu na si kwamba jeshi limeingia sasa, hapana hatujafikia hatua ya kuingiza jeshi.
“Na wananchi karibu nchi nzima wamesikia kinachoendelea hapa Njombe na wengine wametiwa hofu si Tanzania tu, mpaka nje ya mipaka yetu taarifa zimesambaa,” alisema Jenerali Mabeyo.
Alisema kamati ya ulinzi na usalama baada ya matukio hayo ilipeleka timu maalumu mapema iweze kushirikiana na vyombo vilivyopo Njombe kufanya uchunguzi makini na wa kina.
Kutokana na matukio hayo, amewataka wananchi kutulia kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi yake vizuri kuhakikisha waliohusika wanabainika.
Alisema sababu ya kutekeleza mauaji hayo zinafahamika na taratibu za sheria zitachukuliwa dhidi ya wahusika wote wa matukio hayo.
“Ninachosema kwa sasa pasiwepo na hofu, suala hili ni la taifa zaidi, linahusu pengine familia moja moja, sababu zinajionyesha kabisa ni za familia zaidi,” alisema.
Mkuu huyo wa majeshi, alisema suala hilo lazima litakomeshwa na si Njombe pekee bali nchi nzima katika maeneo mengine yenye matukio kama hayo kwa imani potofu kwa wananchi inayotaka kuanza kujengeka.
Aliwataka wananchi waendelee kufanya kazi zao kama kawaida kwa vile kwa sasa vyombo vya dola vinatekeleza majukumu yake.
Alisema vyombo vyote vya dola vinashirikiana kujua ni kina nani waliohusika, sababu za kuhusika na mbinu zilizotumika na watekelezaji wa mauaji hayo.
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Renatha Mzinga, alisema hadi sasa watuhumiwa 30 wanashikiliwa kwa kuhusika kwao na utekaji na mauaji ya watoto hao.
Alisema jalada la watuhumiwa hao lipo kwa mwanasheria na muda wowote akikamilisha utaratibu wa sheria watafikishwa mahakamani.