27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Sera ya JPM kuhusu viwanda yazaa matunda

JUSTIN DAMIAN, DAR ES SALAAM

SERA ya Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda imeanza kuzaa matunda baada ya Kampuni ya Mafuta ya Total kuzindua kiwanda kipya cha kutengeneza vilainishi vya mitambo na magari nchini.

Kampuni hiyo pia inatarajia kutoa ajira kwa vijana hivyo kuchagiza mzunguko wa fedha.

Kwa kuanzia imekwisha kutumia Dola za Marekani zaidi ya milioni 200 kujenga vituo vya mafuta vya Total   nchini Tanzania na nyingine zaidi ya Dola milioni 20 kujenga kiwanda cha vilainishi. 

Kutokana na uwekezaji huo, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kupata kodi isiyopungua Dola za Marekani milioni 2 ( Sh bilioni 2.294) kwa mwaka.

Hayo yalielezwa na Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo wa Masoko na Huduma kwa Afrika Mashariki na Kati,, Jean Torres.

Alikuwa akizungumza kwenye  uzinduzi wa kiwanda cha kisasa cha uchakataji wa vilainishi vya magari na mitambo kilichogharimu Dola za Marekani milioni 20, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Torres alisema Total imeridhishwa na mazingira ya uwekezaji Tanzania   na uungwaji mkono kutoka serikalini, jambo ambalo limewashawishi kuwekeza na kutaka kuwekeza zaidi.

  Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo  nchini, Tarik Moufaddal, alisema kiwanda hicho cha kisasa kitachakata vilainishi vya magari na mitambo ambavyo vitaifanya Tanzania kujitosheleza na hivyo kutokuwa na haja ya kuagiza vilainishi kutoka nje.

Alisema kiwanda hicho kipya kitazalisha metriki tani 15,000 za vilainishi kwa mwaka na hivyo kuwa na  ziada ambayo itasafirishwa katika masoko ya nje ya nchi.

“Kiwanda hiki pia kitatengeneza ajira zaidi ya 80 kwa watu wenye ujuzi wa aina mbalimbali, jambo ambalo litasaidia kutoa ujuzi na maarifa mapya kwa Watanzania.

“Kiwanda pia kitakuwa na programu ya kuwachukua wahitimu wa vyuo vikuu kwa kujifunza kwa vitendo pamoja na kufanya kazi,” alisema.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda, aliishukuru kampuni hiyo kwa kuendelea kuwekeza Tanzania.

Aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwapa kila msaada watakaouhitaji kwa ajili ya kuendeleza uwekezaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles