LAGOS, Nigeria
JENGO la Tume ya Uchaguzi nchini hapa, limeteketea moto zikiwa ni takriban siku sita kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wa msemaji wa tume hiyo, jengo hilo ambalo lipo katika Jimbo la Plateau liliteketea jana na kuunguza vitu vyote muhimu katika uchaguzi huo yakiwamo makasha na karatasi za kupigia kura.
Msemaji huyo alisema njama hizo ni kutaka kukwamisha shughuli hiyo ya upigaji kura, lakini akakaririwa na gazeti la This Day akisema bado ni mapema kuwatuhumu wahusika.
Uchaguzi huo mkuu unatarajiwa kufanyika Jumamosi ijayo na jana Rais Muhammadu Buhari alionya kuhusu kuwapo vitendo vya rushwa.
Katika hatua nyingine, Mshirika mkuu wa Rais Muhammadu Buhari katika uchaguzi mkuu ujao nchini hapa, amewatishia raia wa kigeni akisema yeyote ambaye atajaribu kuingilia mchakato huo atarejeshwa nyumbani kwao akiwa ndani ya mfuko wa kuhifadhia maiti.
Nasir El-Rufai,ambaye ni Gavana wa Jimbo la Kaduna,alitoka kauli hiyo juzi katika mahojiano na Kituo cha Televisheni ya Taifa ilipoanzishwa mada kuhusu jukumu la jumuiya za kimataifa katika uchaguzi huo.
Mada hiyo iliibuka kutokana na kuwapo kelele za jumuiya za kimataifa kutoka Juamuiya ya Umoja wa nchi za Ulaya (EU), Marekani na Uingereza kuhusu kusimamishwa kazi Jaji Mkuu, Walter Onnoghen kwa tuhuma za kuvunja kanuni za utawala bora.
“Tunamsubiri mtu yoyote ayakayejitokeza na kuingilia uchaguzi atarejea nyumbani akiwa kwenye mfuko wa kuhifadhia maiti kwani hakuna aliyekuja Nigeria na kutelekeza jinsi ya kuendesha nchi yetu,”alisema El-Rufai katika mahojiano hayo kuhusu uchaguzi huo wa Februari 16 mwaka huu.
“Tulipata uhuru wetu na tunajaribu kuiendesha nchi yetu vizuri kadri iwezekanavyo,”aliongeza gavana huyo.
Uchugazi huo katika taifa hilo ambalo ni wazalishaji wakubwa wa mafuta unawakutanisha Rais Buhari ambaye aliingia madarakani mwaka 2015 na kiongozi mkubwa wa upinzani, Atiku Abubakar ambaye ni makamu wa rais wa zamani.
Ushindano wao unaonekana kuongeza katika wiki chache zilizopita.
Mwaka jana viongozi hao wawili walisaini makubalino yanayoonyesha watajitolea kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani.