30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Magufuli: Sitawaangusha

01NA BAKARI KIMWANGA, KONDOA

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema hatawaangusha Watanzania kama wakimchagua kuwa rais.

Amesema anatambua changamoto zinazolikabili Taifa na watu wake ikiwa ni pamoja na kuhitaji mabadiliko ya kweli serikalini.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika katika wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, anakerwa na usumbufu wanaoupata wananchi ikiwamo suala la ushuru na kodi za kero kwa mama lishe na waendesha bodaboda ambao wamekuwa wakijiajiri wenyewe.

“Ninajua watu wamekata tamaa kwani haiwezekani kila siku ni kero ya ushuru na kodi kwa mama lishe, bodaboda na wajasiriamali wadogo. Hili silikubali hata kidogo na Serikali ya Magufuli itafunga ushuru na kodi hizi kwa Makufuli.

“Huwezi kuendesha Serikali huku watu wanaonewa, ndiyo maana nasema mimi nitakuwa rais wa wanyonge waliokata tamaa, ninawaomba Watanzania mniamini kwa kunipa kura nyingi ili niwafanyie kazi na naapa kwa jina la Mungu, sitawaangusha,” alisema Dk. Magufuli.

Apokewa na mabango

Akiwa wilayani Chemba, Dk. Magufuli alipokewa na wananchi waliokuwa na mabango wakiomba kulipwa fidia ya ardhi yao.

Baada ya kuona mabango hayo, alimwita mgombea ubunge, Jimbo la Chemba, Juma Nkamia asome mabango hayo kwa sauti.

Kutokana na hali hiyo, Nkamia alisoma mabango hayo yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali kama tunataka maji, fidia ya ardhi kwa maeneo yaliyopitiwa na barabara.

Baada ya hatua hiyo, Dk. Magufuli alisema suala la fidia ni lazima kwa wananchi ambao wamefuatwa na barabara.

“Suala la maji ni lazima, ninaomba mniachie ila kwa suala la fidia kama kuna mtu amefuatwa na barabara na kupita zile mita 22.5 ni lazima mlipwe, lakini kama kuna aliyeifuata barabara ajue hatalipwa.”

Amuombea msamaha Nkamia

Dk. Magufuli alilazimika kumuombea msamaha Nkamia mbele ya wananchi wa vijiji vya Kwa Mtoro na Farkwa baada ya wananchi hao kuguna alipokuwa akimnadi.

“Ndugu zangu ninamuombea msamaha Nkamia (Juma) kama amewakosea, mimi namjua, naomba mumchague kwani alikuwa mwanafunzi wangu Sengerema Sekondari, nasema nimemfundisha,” alisema.

Pamoja na hayo, alisema amejipanga kuhakikisha anaijenga Tanzania mpya yenye mabadiliko ya kweli na kwamba anaomba urais ili akafanye kazi ya kweli ya kuwatumikia Watanzania kwani uzoefu alionao ndani ya Serikali unatosha kwa nafasi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles