MANCHESTER, ENGLAND
WACHEZAJI wa timu ya Manchester United, wanampigia debe kocha wao wa muda, Ole Gunnar Solskjaer, kupewa mkataba wa kudumu huku wakiamini anaweza kuwafanya wapiganie ubingwa msimu ujao.
Kocha huyo amepewa jukumu la kuifundisha timu hiyo kwa kipindi cha miezi sita hadi mwishoni mwa msimu huu huku wakitafuta kocha wa kudumu, lakini kutokana na mwenendo wa timu hiyo tangu apewe inaonekana kuwa bora zaidi.
Kutokana na hali hiyo, idadi kubwa ya wachezaji wamekuwa wakimpigania kocha huyo apewe mkataba wa moja kwa moja mara baada ya kumalizika kwa msimu huu.
Manchester United haijafungwa hata mchezo mmoja tangu iwe chini ya kocha huyo huku akiwa ameisimamia jumla ya michezo 10 na kushinda michezo tisa na kutoka sare mchezo mmoja.
Kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino, amekuwa akihusishwa kuja kuwa kocha mkuu ndani ya Old Trafford, lakini nyota wa Man United, Jesse Lingard, ameweka wazi kuwa, wachezaji wenzake wanataka Solskjaer aachiwe timu kutokana na uwezo wake.
“Solskjaer na Mike Phelan, wamefanikiwa kuirudisha Manchester United katika ubora wake. Wanaijua vizuri Ligi ya Uingereza pamoja na klabu yenyewe kwa ujumla.
“Hadi sasa hakuna mtu ambaye anamkosoa mchezaji huyo, mara zote amekuwa akituambia kwamba, tuna matarajio makubwa sana, hivyo lazima tuhakikishe tunayafikia, ili tuweze kuyafikia lazima tucheze kama United.
“Tuna imani kubwa ya kuja kupigania ubingwa msimu ujao endapo tutaendelea kuwa na kocha huyo na kufanya kile ambacho tunakifanya kwa sasa. Kikubwa ambacho tunakifurahia ni matokeo tunayoyapata,” alisema Lingard.
United inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi huku ikiwa na pointi 48 baada ya kucheza michezo 25, wakati huo wapinzani wao Manchester City wakiwa wanaongoza ligi kutokana na idadi kubwa ya mabao, lakini wapo sawa na Liverpool ambapo wote wana pointi 62.