Bethsheba Wambura, Dar es Salaam
Rais Dk. John magufuli amesema katika utawala wake hajawahi kumpa mtu yeyote mipaka ya kuzungumza ila tu anawata watu wanapotoa maoni yao wazingatie sheria za nchi.
Ameyasema hayo leo, Februari 5 alipokuwa akijibu swali la mmoja wa wafanyakazi wa Channel Ten, John Dachi aliyeuliza kama Rais Magufuli ametoa mipaka ya watu kuzungumza hasa waandishi wa habari katika vipindi na habari wanazoandika .
Rais Magufuli, ametembelea kampuni ya Africa Media Group inayomiliki kituo cha Televisheni cha Channel Ten na na redio ya Magic FM katika maadhimisho ya miaka 42 tangu kuanzishwe kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho sasa ndo wamiliki halali wa kampuni hiyo.
“Mimi sijampa mtu mipaka ila nataka kila mtu azungumze kwa kuzingatia sheria na hiyo ndiyo mipaka yetu, vyombo vya habari vizungumze ukweli kwasababu vinatusaidia kufikisha ujumbe kwa wananchi.
“Ukizungumzia mtu vibaya katika vyombo vya habari unaharibu maisha yake bila kujua kama umeyaharibu hakuna mtu anawazuia kufanya kazi zenu ila fanyeni kazi kwa kuzingatia uadilifu na maadili ya uandishi wa habari,” amesema.
Aidha Rais Magufuli ameuagiza uongozi wa Kampuni hiyo kupunguza matumizi ili fedha zinazopatikana zitumike kuboresha miundombinu itakayowawezesha kuangaliwa na kusikika ndani na nje ya nchi.