30.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi akutwa chini ya uvungu wa kitanda


Na DERICK MILTON-BARIADI

MWANAFUNZI wa kike wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Ikinabushu wilayani Bariadi, (jina linahifadhiwa),  amekutwa chini ya uvungu wa kitanda nyumbani kwa bibi yake.

Mwanafunzi huyo alikutwa kwenye eneo hilo akiwa hajitambuai baada ya kupotea kwa   siku tano tangu Januari 25,  2019 mpaka jana.

Inaelezwa kuwa  alikutwa chini ya uvungu wa kitanda cha bibi yake katika mazingira ya kutatanisha.

Tukio hilo lilikusanya umati wa watu katika Kijiji cha Ikinabushu huku wengine wakihusisha tukio hilo na imani za ushirikina.

Mwanafunzi huyo alikuwa akiishi na bibi yake aliyefahamika kwa jina Kwandu Kiluma (70), wadogo zake wawili, kaka yake na mama yake wa kambo.

Akizungumza mbele ya wananchi waliofika kushuhudia tukio hilo, kaka wa mwanafunzi huyo, Samson Lambo, alisema alipokea taarifa kutoka baba yake mdogo anayeishi mkoani Kigoma juu ya kupotea mdogo wao.

“Alinipigia simu baba yangu mdogo akinieleza kupotea kwa huyu mdogo wetu, nikaja hapa nyumbani kuwauliza waliopo, wakanieleza toka Ijumaa alipoondoka kwenda shule lakini hakurejea, tukaanza kufuatilia tukatoa taarifa shuleni na serikali ya kijiji.

 “ Lakini wakati tunaendelea kufuatilia huku na kule, hawa watoto wadogo wanaoishi hapa wakanieleza kuwa juzi walimuona kwenye ghala la chakula lililoko hapa nyumbani.

“Walisema  walimuita akakataa na badala yake akaingia ndani ya hilo ghala na kupotea,”  alisema Lambo.

Kaka  wa mwanafunzi huyo, alisema  baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa watoto hao zilizoongeza utata wa kupotea mdogo wao, walikaa kikao cha familia na kuamua kutafuta njia mbadala ya kuhakikisha wanampata.

Alisema waliamua kumwita mganga wa tiba  za asili kutoka katika kijiji chao kwa ajili ya kuwasaidia.

Alisema  mganga huyo alitengeneza dawa zake na kuwaleleza kuwa mdogo wao yupo ndani ya nyumba yao.

“Baada ya kutengeza dawa zake huyo mganga na sisi tukiwa tunashuhudia, alitwambia tuingie ndani na kuangalia chini ya uvungu mwa kitanda anacholala bibi yetu na kumkuta mdogo wetu akiwa amelala,” alisema.

Alisema  baada ya kumkuta eneo hilo, walimtoa nje na kuzungumza naye huku akiwaomba maji ya kunywa pamoja na chakula na walimkuta akiwa na madaftari yake ya shule.

Lambo alisema awali wakihangaika kumtafuta mdogo wao hadi kwenye hilo ghala la chakula walikumbana na idadi kubwa ya paka ambao alisema walikuwa wanazidi 50 huku wakiwa wamezunguka ghala hilo.

KAULI YA BIBI

Bibi wa mwanafunzi huyo aliyetajwa kwa jina la Kwandu, alikiri mjukuu wake kukutwa uvunguni mwa kitanda chake, huku akidai   hahusiki  na kupotea kwa mwanafunzi huyo.

“Hata mimi nilikuwa najiuliza ni wapi amepotelea? Kila siku hapa nyumbani tulikuwa tunamtafuta…

“Lakini mimi sihusiki na kupotea kwake, wala kukutwa kwenye kitanda, nahisi kuna watu wamehusika lakini wamepitia kwangu   nionekane mimi kuwa ni mchawi,” alisema Kwandu.

Kuhusu paka waliokutwa kwenye ghala la chakula, alisema  paka hao ni kawaida kuwapo eneo hilo huku akibainisha kuwa kazi yao ni kukamata panya ambao wapo wengi nyumbani kwake.

MWANAFUNZI

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo la tukio hilo, mwanafunzi huyo (jina linahifadhiwa) alisema   hajui jinsi alivyopotea katika mazungira hayo lakini alikuwa anajiona yuko kitandani kila siku amelala.

Alisema   akiwa kitandani alikuwa akiona amezungukwa na watu wengi wanaume kwa wanawake huku wakiwa wamevaa mavazi meupe na mekundu akiwamo bibi yake.

“Mimi kila siku nilikuwa najiona kama naenda shule na kurudi nyumbani kama kawaida.

“Ila hapa nimeambiwa kuwa toka shule zimefunguliwa sijawahi kufika shuleni na daftari zangu hazijaandikwa kitu, lakini mimi nilikuwa naingia hadi darasani na kuandika,” alisema Mahila.

MWALIMU ALONGA

Mmoja wa mwalimu wa mwanafunzi huyo, Masumbuko Juma alisema tagu shule zimefunguliwa Januari 7, mwaka huu, mwanafunzi huyo  hakuwahi kuhudhuria shuleni.

Alisema pamoja na familia yake, wamekuwa wakifika shuleni hapo kwa lengo la kufuatilia ni wapi alipo mwanafunzi huyo ambaye hakuonekana tangu shule zilipofunguliwa.

MWENYEKITI WA KIJIJI

Mwenyekiti wa Kijiji hicho,  Masanja Busalu alikiri kutokea   tukio hilo ambalo alieleza ni mara ya kwanza   katika kijiji chake na ni jambo la ajabulililowashtua watu wengi.

Alisema matukio kama hayo hayakubaliki kwenye jamii, na hata serikali haitambui masuala ya ushirikina, huku akiiomba serikali kumchukua bibi huyo   wananchi wasiweze kumdhuru.

POLISI

  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Deusdedit Nsimeki, alisema wanamshikiria bibi wa mwanafunzi huyo kwa mahojiano zaidi. Alisema wanamshikilia bibi huyo kutokana na kutuhumiwa  kujihusisha na vitendo vya ushirikina na uchunguzi utakapokamilia hatua dhidi yake zitachukuliwa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles