30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Edward Lowassa aiteka tena Dar

lowasaMAELFU ya wakazi wa   Dar es Salaam jana waliacha shughuli zao zote na kujiunga katika msafara wa mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ambaye alikuwa na mikutano ya kampeni  katika majimbo ya Temeke, Segerea, Ubungo na Kawe.

Lowassa aliwasili Temeke katika Uwanja vya Mwembeyanga saa 05:20 asubuhi ambako alilakiwa na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza.

Akifuatana na Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye   alishuhdia wananchi waliokuwapo uwanjani hapo, muda wote wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu mgombea huyo wa Ukawa.

“Rais…Rais…Rais…tuna imani na wewe Lowassa, tumechoshwa na CCM, Lowassa wewe ndiye tegemeo letu…kura zetu umepata, angalia ulivyo tishio, unakitesa chama ulichokiacha…Ikulu sasa ni yako,” waliimba wananchi hao.

Baada ya mkutano huo wa Mwembeyanga, Lowassa na msafara wake walielekea  Segerea ambako vijana watembea kwa miguu  na waendesha pikipiki (bodaboda) na bajaji walisindikiza msafara huo na kusababisha magari yote katika barabara za Sokota na Maendela hadi Buguruni kutokupitika.

Msafara huo uliwasili huo uliwasili katika Uwanja wa Shule ya Shule ya Msingi Liwiti na kukuta umati   wa watu umefurika  ukiwa na shauku ya kumuona.

Baadhi ya wananchi waliofika kwenye uwanja huo   walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe:  ‘Lowassa kwanza familia baadaye’, ‘Magufuli jiandae kuwa mlinzi wa Lowassa’, ‘Uwezo tunao sababu tunazo wananchi tunahitaji mabadiliko’ na ‘Segerea ni Mtatiro tu wengine nendeni mkaendelee na urembo wenu’ na mengineyo.

Hata hivyo, wakati Lowassa anapanda jukwaani kuhutubia, ghafla lilitokea kundi kubwa la wananchi ambao walitembea kwa miguu kutoka Temeke huku wakirukaruka na kuimba:  “Rais…Rais…Rais…tumeamua tukufuate huku huku, sasa waseme kama unatupa hela…tumekufuata kwa mapenzi yetu, angalia tulivyo wengi, acha wao wajaze wasanii na kuwabeba watu kwenye malori sisi tumetembea kwa miguu yetu kutoka Temeke,”.

Saa 07:45 Lowassa na msafara wake walimaliza kuwahutubia wananchi hao na   ulianza safari kuelekea Manzese katika Uwanja wa TP Uzuri Sinza kupitia barabara ya Mandela hadi Ubungo.

Msafara huo ulifunga barabara za Tabata, Mandela na baadaye Morogoro eneo la Ubungo ambako umati mkubwa wa watu pamoja na waendesha bodaboda wa maeneo hayo  nao walijiunga kwenye msafara huo na kuufanya kuzidi kuwa mkubwa.

Ulipofika   Ubungo, umati mkubwa wa watu ulikuwa umefurika pembezoni mwa barabara ya Mandela huku wakishangilia na kunyoosha vidole viwili juu,   alama ambayo hutumiwa na Chadema.

Nyimbo mbalimbali ziliendelea kuimbwa na wananchi hao   wengine wakimtaka Lowassa asimame  na kuwapungia mikono. “Rais… Rais… Rais… tunaomba tukuone, sisi malofa, wapumbavu  na masikini wewe ndiye mkombozi wetu,” waliimba wananchi hao.

Wakati hayo yakiendelea,  barabara zote katika eneo la Ubungo zilifungwa   kwa zaidi ya dakika 20, ndipo Lowassa alipoamua  kusimama na kuwapungia mkono wananchi hao.

Lowassa aliendelea kusimama kwenye gari lake la wazi hadi eneo la Shekilango, Sinza kuelekea viwanja vya TP Uzuri Sinza ambako pia alihutubia mkutano mkubwa wa kampeni kabla ya kuondoka tena kwenda Viwanja vya Tanganyika Peackers katika Jimbo la Kawe.

Kama ilivyokuwa maeneo mengine, umati mkubwa wa wananchi hao waliokuwapo katika viwanja hivyo nao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali  zikiwamo: “Lowassa wewe tayari ni rais wetu, angalia tumeacha kazi zetu tumekuja hapa tangu asubuhi ili tukusikilize, huyo Magufuli si anajidai anajua ubodigadi sasa tunaomba aje kuwa mlinzi wako…”

Nacho kikundi kingine cha vijana kilikuwa kikiimba: “Huyo Masaburi (Didas, aliyekuwa meya wa Dar es Salaam na sasa anagombea ubunge Ubungo kwa tiketi ya CCM) akaombe kura Magogoni…sisi hatumhitaji, kasababisha watu wafe kwa kipindupindu, yeye kanenepa halafu eti anataka tumchague awe mbunge wetu… hizi si dharau jamani?  Tutamchague Kubenea kuwa mbunge wetu wa Ubungo na rais wetu ni wewe Lowassa”.

Kikundi kingine cha vijana walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali huku wengine wakiitikia kwa kibwagizo cha ‘Lowassa kama Ronaldo’, Lowassa tukikuona tunachanganyikiwa kabisa, Magufuli hana hata mvuto…yaani wewe nyota yako ni hatari,’.

Ahadi za Lowassa

Akiwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Liwiti,  Lowassa alishindwa kuzungumza kwa muda kutokana na furaha aliyoiita mahaba, baada ya kukuta umati mkubwa umefurika.

Kabla ya kuwasalimia wananchi, Lowassa alijikuta akitabasamu na kushindwa kuzungumza kwa sekunde kadhaa huku umati wa wananchi hao wakiendelea kumshangilia.

“Jamani haya ni mapenzi au mahaba… nina furaha isiyo kifani na ninasema hivi umati huu na shangwe hizi ni salamu kwa  Chama Cha Mapinduzi (CCM)… napenda kuwapelekea salamu kuwa wananchi wamenipokea kwa shangwe na wanahitaji mabadiliko,”alisema Lowassa huku akishangiliwa.

Alisema, “mkusanyiko huo ni salamu tosha  kwa CCM kuwa mnahitajika mabadiliko na mimi nawaomba mnipe kura na mzilinde”.

Lowassa alisema anauchukia umaskini na kueleza kuwa baada ya miaka 50 ya uhuru sasa wananchi wanahitaji hali bora na wataipata kupitia Ukawa na si   CCM.

“ Ninachukia umaskini ndugu zangu…nawaambia hivi nitaongoza nchi kwa spidi 120… ambaye hataweza kwenda na kasi yangu ataachia ngazi yeye mwenyewe,” alisema.

Alisema anawashukuru wauguzi na madaktari ambao wameona umuhimu wa mabadiliko baada ya kuvutana na hatimaye wamekubali matokeo na kuona hakuna namna mabadiliko yanahitajika.

Lowassa alisema akiingia Ikulu siku 100 za mwanzo za utawala wake atahakikisha ameimarisha mambo 11 ambayo yamekuwa  kero kwa wananchi.

Alitaja vipaumbele vyake kuwa ni mfumo bora wa kodi, kuundwa kwa tume ya kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, kupunguza kodi kwa wafanyakazi, kuongeza maslahi ya Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), kuondoa kodi za wafanyabiashara ndogondogo na bodaboda na kufuta ada kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu.

“Uwezo tunao na nia tunayo.. ndugu zetu CCM salamu ni hizi, wazipate kuwa hawawezi kuzuia mafuriko haya kwani wameunda mfumo wa Teknohama kwa ajili ya kuwakomesha watoto wa maskini lakini mimi nitaweka usawa kwa wote kupata elimu bora,”alisema Lowassa.

MNYIKA

Naye Mgombea ubunge waKibamba  kwa tiketi ya Chadema, John Mnyika alisema wanachokifanya sasa ni kuzuia bao la mkono kwa kuwa rais tayari wanaye.

Alisema Mwenyekiti wa   Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva kueleza kuwa Chadema inawapa shida anakosea kwa sababu  wanaompa shida ni wananchi ambao wanahitaji mabadiliko.

Mnyika alisema hadi ifikapo Oktoba 4   mwaka huu, NEC iwe imetoa utaratibu wa kueleweka kuruhusu wataalam wa Ukawa  waupitie mfumo wa upigaji kura katika kompyuta zikazotumiwa katika Uchaguzi Mkuu   wa Oktoba.

“ Ni lazima tujihakikishie mfumo wa kompyuta zao kama tulivyoomba ili kudhibiti bao la mkono vinginevyo.. hatutakubali ikifika hiyo Otoba 4 mwaka huu,’’alisema Mnyika.

SUMAYE

Waziri Mkuu Mstaafu,  Frederick Sumaye alisema zaidi ya mikoa 20 aliyopita wananchi wanahitaji mabadiliko na CCM haina historia ya kukumbukwa zaidi ya kuwakandamiza wananchi kwa miaka 50 yao.

“Huyo Magufuli, mgombea wa CCM akiwa rais ni maumivu tu, mtu ambaye anafanya uamuzi kwa kulipuka bila kuangalia athari wakati akiwa waziri, itakuwaje akiwa rais?

“Huyo huyo Magufuli alivunja majengo ya Wakala wa Barabara (TANROADS) Ubungo, lakini sasa eneo hilohilo hivi sasa linajengwa jengo jingine, hivi eneo hilo limehama au bado lipo?” aliuliza Sumaye huku wananchi wakiitikia, “bado lipo…”

“ Hadi sasa nchi inadaiwa Sh trilioni 45… madeni kutoka nje ni jambo la aibu sana na mkumbuke mkimchagua mgombea wao kitakachofuata ni kulipa madeni tu,”alisema Sumaye na kuongeza:

“Kuna deni la wakandarasi zaidi ya Sh bilioni 900 tunadaiwa… ninawaambia kuwa tukifanya kosa CCM wakarejea madarakani tutakuwa tunajiangamiza sisi wenyewe”.

Mbowe awataka vijana kukesha

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe aliwataka watanzania kukesha wakijiandaa na kutafakari siku ya kuamkia kupiga kura ili kuanza maandalizi safari ya uhakika itakayorudisha heshima ya nchi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni kwenye viwanja vya Tanganyika Parkers jana, Mbowe alisema usiku wa oktoba 24 siyo siku ya kulala kwa kuwa ni siku ya ukombozi wa taifa.

“Tarehe 24 siyo siku ya kukesha disco, ni siku ya kufanya maandalizi ya ukombozi wa taifa hili, hakuna kurudi nyuma baada ya kupiga kura, piga hatua 100 kutoka kituo cha kura halafu linda kura….hakuna kulala mpaka matokeo ya udiwani, ubunge na urais yatangazwe, tutakesha hadi matokeo ya urais yatangazwe,” alisisitiza Mbowe.

Mbatia akanusha uvumi wa ushirikina

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Umoja huo, James Mbatia alikanusha uvumi ulioenea katika mitandao ya jamii na maeneo mbalimbali nchini kuwa amekamatwa akiwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi akiwa na fuvu la kichwa cha mtoto.

“Mimi na familia yangu ni wacha Mungu hatuamini katika ushirikina nimekulia katika familia ya wacha Mungu hivyo siwezi kufanya kitu kama hicho labda wao CCM, maana wao ndiyo waliotengeneza picha hiyo na kuiweka mitandaoni,” alisema Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

Habari hii imeandaliwa na Elizabeth Hombo, Christina Gauluhanga, Tunu Nassoro na Adam Mkwepu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles