Upendo Mosha, Hai
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro Helga Mchomvu, amekanusha taarifa za Mkuu wa Wilaya hiyo kumnyang’anya Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe na kudai kuwa amepotosha umma.
Hivi karibuni Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, alitangaza kumnyang’anya mbunge huyo ofisi na kuikabidhi kwa maofisa uhamiaji kwa madai kuwa Mbowe hajaitumia tangu mwaka 2010 alipochaguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Januari 18, katika ofisi ya Mbunge, iliyopo katika maeneo ya Mji Mdogo wa Bomang’ombe, wilayani humo Mwenyekiti huyo, amedai taarifa za Mbunge kunyang’anywa ofisi si za kweli na kwamba Mkuu huyo wa wilaya aliudanganya umma.
“Taarifa za Mbunge wetu kunyang’anywa ofisi yake na Mkuu wa Wilaya si za kweli, alikuwa na malengo yake ya kisiasa kwani toka Mbowe achaguliwe hajawahi kuwa na ofisi katika Jengo la Mkuu wa Wilaya bali alikuwa anatumia ofisi yake binafsi kuwahudumia wananchi ambayo imejitosheleza,” amesema.
Aidha, amesema kitendo cha mkuu huyo wa wilaya kutangaza jambo hilo kililenga kuwadanganya wananchi kwamba mbunge huyo hatoi huduma za maendeleo kwa wananchi jambo ambalo si la kweli.