33.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Al-Shabaab: Shambulio la Nairobi ujumbe kwa Marekani

NAIROBI, KENYA

KUNDI la wanamgambo wa Somalia lililodai kuhusika na shambulio katika hoteli ya kifahari ya Dusit D2  nchini Kenya na kuua raia 21 limesema huo ulikuwa ujumbe kwa Rais wa Marekani, Donald Trump.

Kundi hilo la al-Shabaab, lenye uhusiano na al-Qaeda, lilisema shambulio lao linatokana na kauli mbaya za Trump pamoja na uamuzi wake wa kutambua Yerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. 

“Kutokana na kauli ya Rais wa Marekani, Donald Trump na tangazo lake la vita, tunayalenga masilahi ya magharibi na Israel duniani na kwa ajili ya kuziunga mkono familia za Kiislamu Palestina,” ilisema taarifa ya kundi hilo.

Katika shambulio hilo la Jumanne watu 21 waliuawa, huku washambuliaji watano nao wakiangamizwa.

kwa mujibu wa Msalaba Mwekundu, watu zaidi ya 700 waliokolewa kutoka jengo hilo baada ya mzingiro wa saa 20, huku wengine 94 waliokuwa wameripotiwa kutojulikana walipo wakiwa wamepatikana jana jioni.

Shambulio hilo lililolaaniwa duniani, linafanana na lile la mwaka 2013 wakati al-Shabaab walipoua watu 67 katika kituo cha biashara cha Westgate jijini hapa.

Al-Shabaab wameapa kuendelea kuishambulia Kenya wakichukizwa na uamuzi wake wa kupeleka askari Somalia kupambana nao tangu mwaka 2011.

Shambulio la Jumanne liliangukia katika tarehe ya maadhimisho ya miaka mitatu wakati al-Shabaab waliposhambulia kambi ya kijeshi ya Kenya na kuua askari zaidi ya 100.

THAILAND WADAI SHAMBULIO NI SABABU YA VYAKULA VYAO VITAMU

Naibu Waziri Mkuu wa Thailand, Prawit Wongsuwan, amedai huenda magaidi waliilenga hoteli hiyo inayomilikiwa na mwekezaji wa taifa hilo kwa sababu ya vyakula vitamu.

Wongsuwan, ambaye pia ni Waziri wa Ulinzi, alitoa kauli hiyo juzi wakati wa mkutano na wanahabari. 

Aliwaambia wanahabari kuwa uzuri ni kuwa hakuna raia wa Thailand aliyeuawa katika shambulio hilo la kutisha. 

Wakati alipoulizwa nini anadhani kilifanya hoteli hiyo inayomilikiwa na Thailand ilengwe na mashambulizi, alijibu; “sijui. Pengine ni kutokana na utamu wa vyakula.” 

Hoteli hiyo ya DusitD2 inamilikiwa na Dusit Thani, himaya inayomiliki hoteli 29 katika mataifa 18.

MAGAIDI WAZUNGUMZA KISWAHILI

Mwanafunzi mwenye umri wa miaka 23, Cyprian Otieno anasimulia kuwa magaidi walizungumza Kiswahili.

Otieno alisema kuwa alienda kukutana na rafiki kwa chakula cha mchana eneo jingine la Westlands, kisha wakaamua kwenda Dusit ambako rafikiye alitaka wakapate kilaji.

“Mara ghafla tukasikia mlio wa bomu ukifuatiwa na wa risasi. Walinzi wa langoni walipaza sauti za kututahadharisha ‘nendeni nyuma, nendeni nyuma’ kwa Kiswahili na Kiingereza,” aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP).

Alisema baadhi walikimbia huku wengine wakijaribu kujificha, wakisubiri kwa nusu saa hadi waliposikia sauti za magaidi zikiunguruma kwa Kiswahili ‘waue, waue, waue’ huku milio ya risasi ikisikika zaidi.

POLISI WAKUTA MABOMU NDANI YA HOTELI

Wataalamu wa mabomu jana waliona mabomu katika eneo la ofisi za Dusit, ambako magaidi walivamia Jumanne.

Kupitia mtandao wa Twitter, Jeshi la Polisi liliutaka umma kutoshtushwa watakaposikia mIlio wakati maofisa wao watakapotegua mabomu hayo.

“Tunapenda kuufahamisha umma kwamba wataalamu wa mabomu kutoka Kurugenzi ya Uchunguzi wa Jinai bado wanaendelea na uchunguzi eneo la tukio kuangalia iwapo kumebakia mabomu au mitego,” ilisema taarifa ya polisi.

SABABU ZA MAGAIDI KUILENGA DUSIT D2

Hoteli ya Dusit D2 ndiyo ilikuwa kitovu cha shambulizi la kigaidi la Jumanne, hali iliyosababisha wengi kuanza kuhoji sababu za magaidi kulenga hoteli hiyo iliyoko kwenye mtaa wa hadhi ya juu wa Lavinghton.

Dusit D2 ambayo ina makao yake makuu jijini Bangkok nchini Thailand, ilifungua tawi lake katika Barabara ya Riverside 14 jijini hapa mwaka 2014.

Hoteli hiyo inayomilikiwa na familia ya Sanghrajka inayomiliki pia biashara za Tile & Carpet Centre, ilishinda tuzo ya ‘The Best Luxury Business Hotel’ mwaka jana katika kanda ya Afrika Mashariki.

Wachambuzi wa mambo walisema huenda magaidi walilenga hoteli hiyo kwa sababu ya kuandaa kongamano na shughuli nyingi zinazohusisha wageni wengi wa kimataifa.

“Magaidi wanapenda mahali ambako kuna wageni wengi  wa kigeni ili maovu yao yawezwe kumulikwa kimataifa. Hata mjini Mogadishu hoteli nyingi zinazoshambuliwa ni zile zenye raia wa kigeni na ofisi za Umoja wa Mataifa,” alisema mtaalamu wa maswala ya usalama, Simiyu Werunga.

Kwa mujibu wa Werunga, ilikuwa rahisi kwa magaidi kupanga shambulio hilo kutokana na shughuli nyingi za wageni zinazoendelea katika hoteli hiyo.

Barabara ya Riverside Drive ina shughuli nyingi kutokana na kuwepo kwa ofisi kadhaa za mabalozi mbalimbali na benki kadhaa.

Aidha eneo hilo pia linatembelewa na idadi kubwa ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

Hata hivyo, mtaalamu mwingine wa masuala ya usalama, Antony Njeru anahisi DusitD2 ilijianika sana kwa kuchapisha habari muhimu za kiusalama katika tovuti yake.

“Inaonekana magaidi walipata ramani yote ya Dusit Complex katika tovuti yao. Ni makosa kutoa maelezo ya kina kuhusu maeneo ya kiusalama ndani ya jengo,” alisema Njeru.

Hoteli hiyo iliyoanzisha mwaka 1948, inamiliki matawi mengine 25 duniani.

Ndani ya DusitD2, kuna mashirika mengine makubwa kama vile Reckitt Benckiser, Amadeus Global Travel Distribution Ltd, Colgate Palmolive (EA) Limited na Cellulant Kenya Limited.

Kampuni nyingine zenye ofisi katika hoteli hiyo ni Brighter Monday Limited, Pernod Ricard, Metta, LG, Redhouse PR, Fanisi Capital, Nielsen, Secret Garden Café, Amadiva Salon, Visa, CRA, Deepa Dosaja na Benki ya I&M.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles