25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Jifunze kuyakubali maisha katika uhalisia wake

Christian Bwaya

Maisha yana vipindi vya majira tofauti. Kuna nyakati za nuru na mvua kutunyeshea. Nyakati za matumaini na furaha.

Nyakati za kupanda na mafanikio. Katika majira kama haya unakutana na mambo yanayokufanya uwe mtu mwenye furaha. Kila unachotamani kifanyike kinatokea.

Uliyetaka akupende anakupenda kupita matarajio yako. Watoto wanafanya vizuri, mwenzi wako anafanikiwa, familia yako imejaa furaha na karibu kila unachokihitaji ili kufanikisha unayoyatarajia kipo ndani ya uwezo wako. Katika nyakati kama hizi unakuwa mtu mwenye furaha. Unakuwa na moyo uliojaa matumaini. Uso wako unakuwa angavu.

Nyakati za nuru zinakufanya utamani kila unayekutana naye angefahamu namna mambo yako yanavyokwenda vizuri. Wapo ambao hutumia mitandao ya kijamii kueleza vile maisha yao yanavyonyooka.

Wataweka picha za watoto wao wazuri, picha za wenzi wao na hata familia zao zenye sura ya kupendeza. Haya ndiyo majira ya nuru. Mvua ya matumaini inakunyeshea na maisha yanakuwa yenye furaha.

Lakini pia, zipo nyakati za giza. Hizi ni nyakati zinazokatisha tama kwa sababu ile nuru uliyokuwa nayo inanywea na nafasi yake kuchukuliwa na giza. Mambo yanakwenda mrama. Maisha yanakuwa kama mlima mkali kwenye miiba na makorongo ya kutisha.

Hizi ni nyakati za kukataliwa na watu uliotamani wawe karibu na wewe. Uliyempenda anakuchukia, na usiyempenda anafanikiwa. Kila unaloligusa halionekani kwenda sawa. Matukio yasiyotarajiwa yanakuandama na mipango uliyonayo inavurugika. Hiki ni kipindi ambacho maisha yanajaa huzuni. Unakata tamaa. 

Unapopita kwenye majira kama haya maisha yanakuwa machungu. Wakati mwingine matumaini kidogo uliyokuwa nayo yanapotea.  Shauri ya kukata tama unaanza kuogopa kukutana na watu. Kukata tama kunakufanya usione jema lolote kwa wanaokuzunguka.

Unakerwa na vitu ambavyo kwa hali ya kawaida visingepaswa kukukera. Unakuwa mkosoaji wa karibu kwa kila unachokisikia. Usiku huwezi kulala kwa sababu moyo unakuwa umejaa kila aina ya mahangaiko. Unapoamka unakuwa mchovu na muda mwingi unabaki kuwa mtu wa kusinzia sinzia. Maisha yanakosa ile ladha yake.

Katika hali kama hii ya kukata tama unafanyaje?

Unajitenga watu ambao, kwa namna moja au nyingine ndio pengine wangekuwa msaada wako? Unajifariji kwa kufurahia upungufu wa watu wengine? Unafanyaje hasa?

Shida zetu nyingi huanzia kwenye kile tunachokiamini. Tunachokifikiri na kukiamini ndicho kinachotufanya ama tukose amani au tuwe na furaha. Maana yake ni kwamba ili kukabiliana na majira ya giza katika maisha lazima kubadili namna ya kufikiri.

Wakati mwingine kile unachofikiri kinakumaliza ndicho kinachokujenga kuwa mtu bora. Jua linapowaka, hicho ndicho huwa kipindi mimea iliyonyeshewa mvua kwa muda mrefu hupumua. Bila kipindi cha jua kuwaka mimea huoza. Majira magumu ni faida kwa mimea.

Ndivyo ilivyo katika maisha. Ili uende mbele lazima upite kwenye mitihani ya maisha. Huenda migogoro uliyonayo kwenye uhusiano wako inakuandaa kufurahia uhusiano wako mbeleni. Inawezekana ulitamani kuolewa na bado hujaolewa.

Unakosa furaha na maisha. Lakini fikiria watu wengi walioolewa na watu waliogeuka kuwa kero kwao. Kutimia kwa ndoto zao za kuolewa hakujawaletea furaha waliyoitarajia.

Namkumbuka dada mmoja aliyekataliwa na mchumba wake siku chache kabla ya harusi. Aliumia. Kilichomuumiza zaidi yule aliyepanga kufunga naye ndoa aliamua kumuoa rafiki yake siku chache baadae. Kama kuna mambo yanaweza kumuumiza mtu, hili ni mojawapo.

Lakini baada ya miezi kadhaa ya ndoa hiyo, iligundulika kumbe kijana yule alikuwa na familia nyingine ya siri. Wakati mwingine unaweza kupoteza amani kwa sababu tu hujui kwanini ndoto yako haijatimia. Ungekuwa na uwezo wa kuelewa kwanini ulichotamani kitokee hakijatokea ungeweza kuwa na furaha.

Labda kinachokunyima furaha ni vurugu kwenye ndoa au kuachika. Ulipokuwa kijana uliota kuwa na ndoa ya mfano. Unapowaona wenzako wakifurahia ndoa zao, unajikatia tama na kujihurumia. Unajiona kama mtu mwenye bahati mbaya kwenye maisha.

Lakini fikiria, unayo mangapi mengine ambayo wengine wangetamani kuwa nayo lakini hawana? Wakati wewe shida yako ni ndoa, wapo wenye ndoa nzuri lakini hawana furaha kwa sababu wanatamani kuwa na kazi nzuri uliyonayo. Wakati wewe unatamani kupata watoto, wapo wengi wenye watoto wavuta bangi, walevi, wahuni, wasiosikia na wakati mwingine hao hao wamewasababishia matatizo makubwa wazazi wao.

Maana yangu ni kwamba tunahitaji kujifunza kuyakubali maisha katika uhalisia wake. Magumu uliyonayo ni sehemu ya maisha yako. Nyakati hizi ngumu tusizozipenda mara nyingi hutufundisha mambo ambayo tusingepitia magumu hayo pengine tusingejifunza. Nitaeleza jambo hili kwa kirefu wiki ijayo panapo uzima.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754870815, Twitter: @bwaya

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles