25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Kutopiga mswaki chanzo upungufu nguvu za kiume

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

WATAFITI nchini China wamebaini kuwa mwanamume asiyepiga mswaki, walau mara mbili kwa siku, yuko hatarini kupoteza uwezo wake wa kufanya mapenzi.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Jinan nchini China, umebaini hilo. Kumbuka kuwa hii ni moja kati ya taasisi za elimu ya juu zenye heshima kubwa katika sekta ya elimu nchini humo.

Ifahamike kuwa tafiti mbalimbali zimebaini kuwa tatizo hilo linawatesa wanaume takribani milioni 200 duniani kote na idadi hiyo imetabiriwa kufikia milioni 322 mwaka 2025.

Kwa mujibu wa utafiti huo, uliowahusisha wanaume 213,076 kutopiga mswaki husababisha ugonjwa wa fizi, ambao unapunguza mara tatu ufanisi wa mwanaume katika kufanya tendo la ndoa.

Katika utafiti huo, wale waliokuwa wakisumbuliwa na matatizo ya fizi, ikiwamo kuuma na kutoka damu, walikiri kushindwa kuwaridhisha wenza wao faragha.

Ikifafanua majibu ya utafiti huo, ripoti hiyo inasema magonjwa ya fizi hupunguza kiwango cha vichocheo (hormone) za ngono.

Kuiweka sawa ripoti hiyo, Mkuu wa timu ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Jinan, Dk. Xincai Zhou, anasema: “Afya ya kinywa inapaswa kupewa umuhimu na madaktari wanapokuwa wakizungumza na wagonjwa wenye tatizo la uzazi.”

Wakati huo huo, inaelezwa kuwa wavutaji sigara, walevi, wagonjwa wa shinikio la damu, wako hatarini kukumbwa na tatizo la kushindwa kufurahia ngono.

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) limewahi kutoa ripoti yake, ikionesha asilimia 50 ya wanaosumbuliwa na changamoto hiyo ni wale wanaosumbuliwa na ugonjwa hatari wa kisukari.

Aidha, tafiti zingine za kitabibu zimewahi kusema umri nao unaweza kuwa sababu. Taasisi inayojihusisha na Magonjwa ya Mkojo (AUA-American Urological Association) ilibaini kuwa watu wanne kati ya 10 wenye umri wa miaka 40 wanasumbuliwa na hali hiyo.

Idadi hiyo ilipanda hadi kufikia watu sita kati ya 10 waliokuwa na umri wa miaka 65. Pia, utafiti wao ulionesha kuwa watu nane kati ya 10 wenye umri wa miaka 75 wanahangaikia tiba ya upungufu wa nguvu za kiume.

Dk. Xincai Zhou anaongeza kuwa mmoja kati ya watu watano duniani anasumbuliwa na tatizo la fizi kutoa damu, kung’oa meno, au harufu mbaya ya kinywa.

“Walau unatakiwa kuwa na utaratibu wa kupiga mswaki mara mbili kwa siku. Pia unatakiwa kujiwekea utaratibu wa kukutana na daktari wa meno mara kwa mara,” anasema msomi huyo.

Tatizo la upungufu wa nguvu za kiume nchini Marekani ni kubwa, takribani watu milioni 30 wanahaha katika vituo vya afya kutafuta tiba.

Ukiacha hilo la kupiga mswaki, Dk. Xincai Zhou anasema: “Kufanya mazoezi, mpangilio wa vyakula, kunaweza kusaidia kumaliza tatizo.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles