23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Safari ya JKCI hadi kujulikana kimataifa

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SAFARI ya kuanzisha hospitali maalumu itakayotoa huduma za uchunguzi na matibabu dhidi ya magonjwa ya moyo nchini, ilianza rasmi mnamo mwaka 1970.

Kipindi hicho serikali ilikuwa ipo chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Wakati huo serikali ilijipanga kwa mikakati madhubuti ikiwamo kusomesha wataalamu watakaotoa huduma hizo pamoja na kuandaa miundombinu na vifaa vya kutosha.

Uimara na uwezo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo ndani na nje ya nchi sasa unavuma kwa kishindo duniani.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili, Mkurugenzi Mtendaji wa  JKCI, Profesa Mohamed Janabi, anasema idadi ya wagonjwa wanaopata huduma ya uchunguzi na matibabu nayo inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.

 “Tumezidi kupiga hatua, takwimu zetu zinaonesha idadi ya wagonjwa tunaowahudumia inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka.

“Mwaka 2015 tulipoanza rasmi kwa mujibu wa sheria tuliona wagonjwa wa nje (Outpatient) 23,000, mwaka 2016 tuliona  wagonjwa nje 53,000, mwaka 2017 tuliona wagonjwa zaidi ya 60,000 na mwaka 2018 tumeona zaidi ya wagonjwa 76,365,” anasema.

Anasema ikijumuishwa miaka hiyo mitatu wameshahudumia wagonjwa wa nje zaidi ya 200,000 na wamelaza (inpatient) wagojwa zaidi ya 11,000.

3330 wapasuliwa

“Ndani ya kipindi hicho tumeweza kuwafanyia upasuaji wagonjwa 3330, mgonjwa mwenye umri mdogo alikuwa na miaka minne na mwenye umri mkubwa alikuwa na miaka 82.

“Ukijumuisha na wale ambao tumewahudumia lakini hawakuhitaji upasuaji, tumeona wagonjwa zaidi ya 250,000 katika kipindi cha miaka mitatu” anasema.

Anasema iwapo taasisi hiyo ingekuwa haijaanzishwa nchini ingeichukua serikali miaka ipatayo minane kufikia idadi hiyo.

“Kila mwaka ilikuwa inapeleka wagonjwa kati ya 200 hadi 350 na wengi wao walikuwa wagonjwa wa moyo, kila mmoja aligharimu kiasi cha sh. milioni 29, utaona tumeokoa maisha na tumeokoa fedha nyingi za serikali,” anasema.

Hali halisi

Anasema magonjwa ya moyo duniani hivi sasa ni tishio, ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo, kulingana na Shirika la Afya Duniani kila mwaka huua watu milioni 18 sawa na asilimia 31 ya vifo vyote.

Anasema WHO linaeleza idadi hiyo ni mara tatu zaidi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Ukimwi ambao unakadiriwa kusababisha vifo milioni tano kila mwaka.

“Kwa mujibu wa WHO, asilimia 75 ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya moyo hutokea barani Afrika na kwamba idadi kubwa ya vifo hutokea huko Latin Amerika na sehemu za Bara la Asia,” anasema Profesa Janabi.

Tegemeo Afrika

Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi hiyo, Dk.  Tulizo Shemu, anasema uimarishaji wa huduma katika taasisi hiyo uliofanywa na serikali hadi kufikia mwaka 2018 umewawezesha kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa wa moyo. Na kwamba ndani ya mwaka huu hakuna hata mgonjwa mmoja aliyepewa rufaa kwenda nje kwa matibabu.

“Haya ni mafanikio makubwa kwani imesaidia kuokoa fedha nyingi za serikali ambazo hutumika kugharamia matibabu kwa wagonjwa ambao hupelekwa nje ya nchi.

“Kwa mwaka wa fedha 2016/2017 wagonjwa wa moyo waliopelekwa nje ya nchi walikuwa 17 tu, kila mgonjwa mmoja aligharimu serikali kiasi zaidi ya Sh milioni 30 za matibabu,” anabainisha Shemu ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa JKCI.

Anaongeza: “Taasisi hiyo kwa sasa imekuwa na jina kubwa kwa sababu ya matibabu ya kibingwa tunayotoa, tunaaminika barani Afrika, hasa Ukanda wa Mashariki na Kati, tunapokea wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali ndani hadi nje ya nchi, hii ina maana kwamba wana imani na huduma tunazotoa.

“Hivi karibuni katika kliniki yangu, nilipokea na kumuona  mgonjwa kutoka Misri, kitendo cha kuja hapa JKCI, kimetupa picha kwamba mataifa mengi sasa yana imani na sisi,” anasema.

Anasema hivi sasa wanapokea wagonjwa wa nje 300 kwa siku, wagonjwa 10 hadi 15 ni wa rufaa na wagonjwa wawili kati ya hao ni kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati.

“Tunatoa mafunzo kwa madaktari mbalimbali ambapo kwa mwaka madaktari wapatao 20 wanapata mafunzo katika taasisi hiyo, hakuna mgonjwa ambaye anaweza kufika na asipatiwe huduma, wagonjwa wote wanatibiwa bila kujali hali zao kifedha.

“Gharama zetu ni za kawaida kabisa lakini hakuna mgonjwa atakosa huduma, tuna wale ambao hawawezi kabisa kugharamia matibabu lakini nao tunawahudumia,” anasisitiza.

Anasema: “Tunaishukuru mno Serikali ya China kwa msaada wao waliotoa, hatuwezi kuzungumzia mafanikio ya JKCI tulipofikia sasa kuaminiwa duniani na kuwa tegemeo Afrika Mashariki na Kati, tukaacha kuitaja China.

“Pamoja na msaada wa jengo bado China imeendelea kutoa msaada mkubwa wa mafunzo kwa madaktari wa JKCI, wanakwenda nchini humo kwa mafunzo kila mwaka pia madaktari bingwa wa moyo kutoka China huja kwetu kutoa matibabu pamoja na kutoa mafunzo.

“Kila baada ya miaka miwili tunapokea madaktari bingwa kutoka China tunakaa nao hapa kwa miaka miwili tukisaidiana kutibu na pia tunapata mafunzo kutoka kwao, pia tuna madaktari wetu wako China kwa mafunzo mbalimbali.”

Daktari wa usingizi kutoka China, Win Chengwei, anasema wanajivunia kwa ushirikiano mkubwa uliopo kati ya serikali yao na Tanzania.

“Binafsi nafurahi kufanya kazi pamoja na madaktari wa Tanzania na kusaidia kuokoa maisha ya watanzania na wagonjwa wan chi mbalimbali wanaofika hapa kupata huduma.

“Nimebobea upande wa huduma ya dawa ya usingizi na huwa natoa mafunzo kwa madaktari wengine, lakini jambo la msingi kuepukana na magonjwa haya ni watu kuzingatia ulaji unaofaa, kufanya mazoezi, kuepuka uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe,” anatoa rai.

Anga la kimataifa

Profesa Janabi anasema: “Katika kuimarisha uhusiano na uboreshaji wa upasuaji wa magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo kwa watoto, mwaka 2018, Tanzania kupitia JKCI iliachaguliwa kuwa kituo cha ufuatiliaji na shirika la International Quality Improvement Collaborative for Congenital  Heart Surgery (IQIC), nchini Marekani.

“Kabla ya kuchagulia kuwa kituo cha mafunzo, Desemba mwaka juzi, Shirika la IQIC ambalo linasimamiwa na Hospitali ya kimataifa ya watoto ya Boston nchini Marekani liliangalia Hospitali ambayo inafanya kazi  zake vizuri katika upasuaji wa moyo kwa watoto na kuomba taarifa ya kazi walizozifanya kwa kipindi cha  miaka miwili iliyopita,” anasema.

Profesa Janabi anasema kwa kutambulika kwake kimataifa na kuwa moja ya vituo 66 kutoka nchi 25 duniani, JKCI itatumika kutoa elimu katika nchi za Afrika.

“Wataalamu kutoka IQIC watakuwa wanakuja kutoa elimu kwa madaktari wetu pamoja na madaktari wengine wa moyo kwa watoto  wa Afrika,” anabainisha.

Anasema katika kliniki ya watoto kila siku wanatoa huduma kwa  wagonjwa kati ya 25 hadi 30 na kulaza mgonjwa mmoja hadi wawili na kwamba zaidi ya asilimia 75 ya watoto wanaofanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo.

“Ikiwamo matundu na magonjwa yanayoshambulia milango  ya mishipa mikubwa na midogo ya moyo, asilimia 25 ni wale ambao walizaliwa salama lakini wameyapata matatizo hayo baada ya kuzaliwa,” anasema.

Safari ilivyoanza

Katika jarida la JKCI la kipindi cha Julai hadi Desemba, toleo namba 001, ukurasa wa pili, inaelezwa serikali ilianza mikakati kwa kuwapeleka wataalamu wawili nje ya nchi kusomea magonjwa ya moyo ambao ni Profesa Idrissa Mtulia na Profesa Willium Mahalu.

Wataalamu hao walipohitimu masomo yao walirejea nchini, hatua hiyo ilifanya ongezeko la madaktari bingwa wa moyo kufikia watatu akiwamo William Makene ambaye alikuwa ni daktari wa moyo wa Mwalimu Nyerere.

Pamoja na hatua hiyo bado ndoto ya kuanzishwa kwa hospitali hiyo haikutimia kwani miundombinu ya kufanyia kazi haikuwapo tayari.

Mwaka 1990 madaktari hao wa moyo kwa kushirikiana na viongozi wa Kitaifa walijadili upya na kufanyia kazi mikakati ya kuanzisha kituo maalum cha matibabu ya moyo na kuhakikisha huduma inakuwa endelevu.

Mikakati ilijumuisha uandaaji wa vikosi kazi maalum ambavyo vilipewa jukumu la kupata uzoefu kutoka nchi nyingine juu ya uanzishwaji na uendelezwaji wa vituo vya matibabu ya moyo.

Hatua hiyo ililenga kutatua changamoto ambazo zilichangia vituo vingi vya matibabu ya moyo kushindwa kutoa huduma endelevu hasa katika Bara la Afrika.

Inaelezwa serikali haikukata tamaa, jitihada ziliendelea ambapo 2005/06 chini ya uongozi wa awamu ya nne ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, idara ya magonjwa ya ndani, wataalamu 26 walipelekwa india kusomea magonjwa ya moyo.

Mikakati hiyo ilizaa matunda kwani mwaka 2008 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kwa kushirikiana na Menejimenti ya MNH ilianzisha idara maalum ya matibabu ya moyo.

Hatua hiyo ililenga kuimarisha matibabu ya moyo huduma ambayo ilikuwa inapatikana chini ya uongozi wa idara ya magonjwa ya ndani.

Wataalamu waliokwenda kujifunza nchini India walirejea 2008 na kuanza kufanya kazi ya upasuaji kwa kutumia chumba cha upasuaji Taaasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), wagonjwa walilazwa wodi namba 12 iliyopo kibasila MNH.

Nuru yachomoza

Ndoto ya kuanzishwa kwa hospitali hiyo ilianza kutimia baada ya ombi lililowasilishwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ambako aliomba kusaidiwa kufanikisha hilo.

China iliridhia ombi hilo na kuchukua jukumu la kujenga jengo lenye gharama ya Sh bilioni 13.6 na serikali ya Tanzania ilitoa Sh bilioni 13 zilizotumika kununua mashine za kisasa, vitanda na vifaa vinginevyo muhimu.

Katika kipindi hicho madaktari waliokuwa wanasoma nchini Marekani, Israel, China, Afrika Kusini na Ulaya walikuwa wameshahitimu masomo yao na kurudi nchini.

Mwaka 2014 Kituo Maalum cha Matibabu ya Moyo kilizinduliwa rasmi na Kikwete.

Ili kuhakikisha kinakuwa na mamkala kamili, uwezo na maamuzi kuhakikisha huduma zinakuwa endelevu, Septemba 5, 2015 hati ya kuanzisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Hati hiyo ilisainiwa kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi, hivyo JKCI ilianza kufanya kazi rasmi kama taasisi inayojitegemea Julai mosi, 2016.

Mchango wa vyombo vya habari

Profesa Janabi anavishukuru vyombo vya habari kwani vimefanya kazi kubwa kuitangaza taasisi hiyo na kuelimisha jamii kuhusu afya ya moyo.

“Leo hii Watanzania wanajua wakipata tatizo la moyo waende wapi kupata huduma, mmefanya kazi kubwa, wafanyakazi wetu nao wanaendelea kufanya kazi kwa bidii, nina uhakika miaka mitatu ijayo tutazidi kujivunia kuwa mfano bora,” anasema.

Katika hafla ya kusherehekea miaka mitatu ya tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo na kuukaribisha mwaka mpya 2019, iliyofanyika Januari 11, mwaka huu, aliwatunuku vyeti waandishi na vyombo vya habari.

Mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa waliotunukiwa cheti cha heshima kwa kutambua mchango wake katika kuelimisha jamii kuhusu afya ya moyo, hii ni awamu ya pili kwa JKCI kumtunuku, awamu ya kwanza ilifanya hivyo mwaka 2016.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles