32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Uhaba vyumba vya madarasa changamoto mpya sekondari

WAANDISHI WETU-DAR/MIKOANI

WAKATI jamii ikiendelea kufurahia matunda ya elimu bila malipo, kumeibuka changamoto mpya ya uhaba wa vyumba vya madarasa kutokana na wanafunzi walio wengi kufaulu mitihani ya darasa la saba, hivyo kuhitajika kuanza kidato cha kwanza katika maeneo mbalimbali nchini.

Taarifa zilizokusanywa na MTANZANIA katika maeneo mbalimbali nchini zimebainisha kuwapo uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa pamoja na matundu ya vyoo hususani kwa shule za sekondari.

ARUSHA

Mkoani Arusha ujenzi wa madarasa katika baadhi ya shule za sekondari za Serikali unaendelea. Hata hivyo wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule 18 watalazimika kusoma kwa zamu ili kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa uliopo kwa sasa.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana wanafunzi wa kidato cha kwanza kuanza kusoma kwa zamu wakati ujenzi wa vyumba vya madarasa ukiendelea.

Kwitega alisema hatua zilizochukuliwa kuanzia jana ni kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu elimu ya msingi wanaanza masomo.

Alisema walikubaliana juzi katika kikao na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa huo kuweka mkakati wa kuhakikisha madarasa yaliyoanza kujengwa yanakamilika katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

Kwa mujibu wa Kwitega, kati ya wanafunzi 33,035 waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana (sawa na asilimia 87 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani huo), 14,316 sawa na asilimia 43 ndio waliopata nafasi ya chaguo la kwanza.

TANGA
Mkoani Tanga shule za msingi na sekondari ambazo zilitarajiwa kufunguliwa mwanzoni mwa wiki hii, baadhi yake zimekumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kukwamisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo ikiwemo uhaba wa madarasa.
Suala hilo limejitokeza katika Wilaya ya Tanga ambayo awali ilikuwa na uhaba wa vyumba 70 vya madarasa.

Hata hivyo kutokana na juhudi mbalimbali zilizofanyika, hivi sasa kuna uhaba wa vyumba 35.

Akizungumza na MTANZANIA hivi karibuni, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa
alisema wanafunzi 1,324 wamefaulu kuingia kidato cha kwanza.

Alisema ili kukabiliana na uhaba huo wamekwishachukua hatua mbalimbali ikiwamo kuwagawanya wanafunzi 40 kila darasa huku umaliziaji wa majengo ukiendelea.

 “Ukiangalia katika changamoto hii ya uhaba wa madarasa 70, nusu yake yapo kwenye hatua mbalimbali za umaliziaji,” alisema.

WILAYA YA MKINGA
Wilaya ya Mkinga hali ni tofauti kidogo, wao wana uhaba mdogo wa madarasa.
Mkuu wa wilaya hiyo, Mark Yona aliliambia MTANZANIA kuwa wilayani kwake hakuna uhaba mkubwa wa madarasa kwani wana upungufu wa madarasa manane tu.
Alisema uhaba huo upo maeneo ya Mtimbwani, Mkinga, Maramba na Duga ambayo kila moja lina upungufu wa vyumba vya madarasa viwili.

Ili kutatua changamoto hiyo, Yona alisema mkurugenzi wa halmashauri amekwisha kutoa
kibali cha kuchangisha fedha na kununua vifaa.

PANGANI
Katika Wilaya ya Pangani hali imekuwa tofauti pengine na maeneo mengine hapa nchini kutokana na taarifa kwamba hakuna uhaba wa vyumba vya madarasa na hivyo wanafunzi waliofaulu wanaweza kupata fursa ya kusoma.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah alisema wilaya yake kwa sasa haina uhaba wa madarasa, hivyo wanafunzi wanaopaswa kuingia kidato cha kwanza watapata nafasi ya kusoma bila shida.

“Labda nikwambie tu kwamba kwa sasa wilaya yetu sisi hatuna uhaba wa madarasa kama ilivyo kwenye maeneo mengine,” alisisitiza Zainabu.

KOROGWE

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Ngasongwa alisema kuwa awali walikuwa na uhaba wa vyumba 51 vya madarasa, lakini kwa sasa mahitaji yao ni vyumba sita pekee.

Alisema mwongozo mpya wa Tamisemi ambao umeelekeza kila darasa liwe na wanafunzi 50 badala ya 45 wa awali, umewasaidia kupunguza mahitaji hayo.

Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Pugu Kinyamwezi wakiwa nje ya shule hiyo, wakishinikiza watoto wao waendelee kusomakatika shule hiyo, Dar es Salaam jana.

MTWARA

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Omary Kipanga, alisema kuwa wamefanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana wakiwa wa pili kimkoa na 34 kitaifa na kupanda kwa zaidi ya asilimia 10.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Kipanga alisema kuwa mwaka juzi wanafunzi walifaulu kwa asilimia 76.6 na mwaka jana kwa asilimia 86.7.

Alisema kuwa hadi sasa halmashauri ina shule 11, mbili zikiwa katika hatua ya umaliziaji na hadi kufikia Aprili mwaka huu zitakuwa tayari na kila moja itapelekewa wanafunzi zaidi ya 80.

“Unajua wanafunzi waliofaulu ni wengi sana na miundombinu haitoshelezi, ipo changamoto kwa kiasi fulani, hili tulilijua mapema tukaweka mikakati ya ujenzi tangu mwezi wa tano mwaka jana.

“Sasa ili kuweza kupunguza hili tatizo tunatarajia kufungua shule mbili mpya ambazo madarasa yameshapauliwa na yataezekwa hivi karibuni.

“Pia tunayo mikakati ya kuongeza madarasa katika shule hizo 11, tutagawanya mikondo vizuri, hivi sasa tunaangalia madawati ili wanapoanza shule kusiwe na mlundikano,” alisema.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Alhaj Mussa Ndazigula alisema kutokana na wananchi kuonesha mwamko wa elimu kumeisukuma Serikali kukamilisha ujenzi wa madarasa na shule mpya.

Mratibu wa shirika lisilo la kiserikali la MTWANGONET, Fidea Luanda alisema kupitia mradi wa PETS wamebaini changamoto nyingi katika elimu hususan miundombinu pamoja na uhaba mkubwa wa walimu.

Alisema katika utafiti huo, baadhi ya shule haziwezi kuhimili kupokea wanafunzi wote waliofaulu mwaka jana licha ya halmashauri ya wilaya kuwa na wanafunzi wa sekondarai wachache.

“Tulipita kwenye baadhi ya shule ikiwemo Msimbati, Ziwani na Madimba, changamoto ya mlundikano darasani si kubwa isipokuwa kuna uhaba wa walimu ambapo tunajiuliza je uwiano wa wanafunzi utakuwa sawia?” alihoji Luanda.

LINDI

Wakati  maandalizi yakitarajiwa kukamilika ili kuruhusu wanafunzi wapya wa shule za msingi na sekondari, wanafunzi 1,266 mkoani Lindi wapo hatarini kuchelewa kuanza masomo ya kidato cha kwanza kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi ofisini kwake mwishoni mwa wiki.

Zambi alisema idadi ya wanafunzi walio na changamoto kubwa ya kuchelewa masomo kutokana na upungufu wa madarasa ni 1,266, kati yao wasichana ni 664 na wavulana 602.

Alisema Halmashauri ya Lindi inaongoza kwa kuwa na wanafunzi 443 ikifuatiwa na Kilwa (434), Ruangwa (262) na Nachingwea (127), wakati Liwale na Lindi Manispaa kukiwa hakuna upungufu wa madarasa.

Alisema kutokana na ongezeko la ufaulu mkoa unakabiliwa na upungufu wa vyumba vya madarasa 39.

Kilwa na Lindi Vijijini vyumba vinavyohitaji ni kati ya 8 hadi 10 kila moja, Ruangwa 11 na Wilaya ya Nachingwea inahitaji vinne.

Zambi alisema licha ya uwepo wa upungufu huo wa madarasa, kwa wanafunzi wa Nachingwea wataanza kusoma kwa kutumia vyumba vya maabara, wakati wakisubiria ukamilishaji wa vyumba ambavyo ujenzi wake upo hatua za mwisho kwa sekondari za Stesheni na Farm Seventeen.

Katika Halmashauri za Liwale na Manispaa ya Lindi, Zambi alisema hakuna upungufu wa madarasa, hivyo wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa wataendelea na masomo yao kama kawaida.

Katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana, wanafunzi19,046, kati yao wavulana 6,788 na wasichana 6,286 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. Kati yao 13,074 walichaguliwa  kujiunga na elimu ya sekondari mwaka huu.

MANYARA

 Wadau wa elimu, wazazi na walezi mkoani Manyara wameombwa kuisaidia Serikali kwa kuchangia ujenzi wa miundombinu ya elimu ili kuepuka changamoto ya vyumba vya madarasa ambalo ni tatizo.

Mwenyekiti  wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Mohamed Kibiki (Chadema), alisema Serikali ina majukumu mengi yakiwamo ya kutekeleza miradi mikubwa kwa wakati mmoja.

Alisema walifanya mikutano na wananchi na kukubaliana kuchangia miundombinu ili watoto wapate elimu katika mazingira yaliyo bora.  

Kibiki alisema ndani ya miezi mitatu wanatarajia kukusanya Sh milioni 129 kutoka kwa wananchi ambao kila kaya itatoa Sh 36,000.

GEITA

Halmashauri ya Wilaya ya Geita yenye shule za msingi 177 za Serikali, imepokea wanafunzi wote 63,470 waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wenye uhitaji wa vyumba 1,410 kwa uwiano wa wanafunzi 45 kwa kila chumba.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ally Kidwaka, alisema wanafunzi wote waliochaguliwa mwaka huu wameanza masomo.

Aidha kwa upande wa sekondari, Kidwaka alisema wilaya ina jumla ya shule za sekondari 30 za Serikali na katika mwaka wa masomo ulioanza 2019,  inatarajia kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 11,325 sawa na vyumba 225 vya madarasa.

“Vyumba 64 vilivyoachwa na wanafunzi wa kidato cha nne 3,200 vitatumika na wanafunzi wa kidato cha kwanza na hivyo kuwa na upungufu wa vyumba 162 sawa na wanafunzi 8,125 kwa uwiano wa wanafunzi 50 kwa kila chumba,” alisema.

Aidha alisema jumla ya vyumba 28 vilivyojengwa kwa nguvu za wananchi vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi katika shule za sekondari zenye wanafunzi 1,400 ambazo alizitaja kuwa ni Bujula, Butobela, Butundwe, Chigunga, Kagu, Katoro, Lubanga, Nyanchiluluma, Nyankongochoro na Nyaruyeye.

Mmoja wa wazazi ambaye mtoto wake alichaguliwa kuingia kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Kalangalala alisema hakukuwa na tataizo lolote wakati wa kuwapokea.

SIMIYU

Wanafunzi 12,584 mkoani Simiyu wameshindwa kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 50.4 ya wanafunzi wote 24,983 waliofaulu.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini jumla ya wanafunzi 24,983 wamefaulu mtihani wa darasa la saba sawa na asilimia 70.68 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani.

Hata hivyo wanafunzi 12, 584 kati ya 24,983 waliofaulu hawajachaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa miundombinu ya shule yakiwamo ya madarasa.

Sagini alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanakwenda sekondari, hivyo aliwaagiza wakurugenzi wahalmashauri zote mkoani Simiyu kufanya jitihadakatika ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu ili wanafunzi wote waliofaulu waweze kuanza kidato cha kwanza Februari 15.

PWANI

Mkoa wa Pwani unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyumba vya madarasa 122 kwa wanafunzi wa shule ya sekondari waliotakiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo wanafunzi 4,731 waliopaswa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wamekosa nafasi, hivyo kubakia nyumbani.

Ofisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Abdul Maulid akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa wa Pwani (RCC) jana mjini Kibaha, alisema ukosefu wa vyumba vya madarasa umetokana na ongezeko la wanafunzi wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza.

Alisema mwaka huu wanafunzi waliofaulu ni 23,170 ambao kati ya hao 18,439 wamepata nafasi kwa awamu ya kwanza na 4,731 wamekosa nafasi kwakuwa madarasa hayatoshi.

Ili kukidhi wanafunzi wote wa mkoa huo kunahitajika madarasa 1,475 wakati yaliyopo sasa ni 1,353 kwa halmashauri zilizopo mkoani Pwani.

Maulid alitaja halmashauri inayoongoza kwa ukosefu wa vyumba vya madarasa kuwa ni Kibaha Mjini yenye upungufu wa vyumba 45 ikifuatiwa na Mafia (32), Chalinze (29), Kibaha Vijijini (27), Kibiti (24), Bagamoyo (23), Rufiji (22), Kisarawe (13) na Mkuranga (3).

Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo ameziamuru halmashauri zote kutenga fedha ili kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wanaendelea na masomo yao kama kawaida.

Ndikilo alisema anataka ifikapo Januari 30 kila halmashauri iwe imekamilisha ujenzi wa madarasa na vyoo na ifikapo Februari Mosi wanafunzi waliokosa nafasi waendelee kusoma.

SERENGETI

Wanafunzi 2,143 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza mwaka huu wilayani Serengeti mkoani Mara wamekosa nafasi kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa.

Akizungumza na MTANZANIA ofisini kwake juzi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Victor Rutonesha alisema wameweka mikakati ya kuhakikisha wananchi na wadau  wanashirikiana kukamilisha ujenzi wa vyumba 39 vya madarasa katika shule za sekondari ili wanafunzi waliokosa fursa hiyo waweze kuanza masomo mapema kabla ya mwezi Machi.

Alisema idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni wengi, hivyo ni vema wananchi, wadau mbalimbali na watendaji wa vijiji wakasimamia ujenzi wa madarasa kwani itakuwa aibu kwa Serikali kuona watoto hawaingii darasani kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa.

Alisema wanafunzi waliofaulu mtihani huo ni 4,846 sawa na asilimia 69.9 na kati yao wavulana ni 2,638 na wasichana 2,208. Waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni 2,703 sawa na asilimia 55.7, kati yao wavulana ni 1,315 na wasichana 1,388.

Alisema kwa takwimu hizo jumla ya wanafunzi 2,143 wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu. Kati yao wavulana ni 1,323 na wasichana 820.

KAGERA 

Wanafunzi 39,545 wamefanikiwa kujiunga kidato cha kwanza mkoani Kagera mwaka huu ambao kati hao wavulana ni 18,553 na wasichana 20,992. 

Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Aloyce Kamamba alisema vinahitajika vyumba vya madarasa 988 na vilivyopo ni 637 tu.

Alisema kuwa madarasa yaliyopo yamechukua wanafunzi 25,499, kati ya hao wavulana ni 12,356 na wasichana 13,143.

“Hadi sasa vyumba ambavyo vimepungua ni 351, hivyo wanafunzi 14,046 wamekosa nafasi ya kujiunga kidato cha kwanza,” alisema.

Kamamba alisema hadi sasa ujenzi wa vyumba hivyo unaendelea katika hatua mbalimbali za ujenzi na ifikapo Machi wanafunzi wote watakuwa wamejiunga na masomo yao ya kidato cha kwanza.

MWANZA 

Wanafunzi 55,330 waliochaguliwa kujiunga masomo ya sekondari Mkoa wa Mwanza wamefanikiwa kupata nafasi katika shule za serikali na binafsi. 

Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Ligola alisema hawana upungufu wa vyumba vya madarasa kwa upande wa sekondari isipokuwa shule za msingi kuna changamoto ambazo wanaendelea kukabiliana nazo. 

Alisema wanafunzi 55,330 waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu wamepata nafasi katika shule 200 za Serikali na 77 za binafsi na tayari wanaendelea kuhakikisha wote wanaanza masomo. 

“Katika mkoa wangu sina uhaba wa vyumba vya madarasa, hata ukiangalia katika taarifa za wizara, Mwanza haimo kabisa isipokuwa changamoto iliyojitokeza sasa ni upungufu wa madawati.

“Kama mkoa tumezungumza na wadau na tayari tumepata mtu ameturuhusu kupasua mbao katika msitu wa Buhindu uliopo Buchosa, Wilaya ya Sengerema ili kutengeneza madawati,” alisema Ligola.  

MARA
Wanafunzi 2,055 wa Halmashauri ya Tarime Vijijini mkoani Mara wamekosa nafasi ya kujiunga  na shule za sekondari kutokana na upungufu wa vyumba 47 vya madarasa.
Hayo yamebainika katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Tarime Vijijini.

Madiwani walisema kuna haja halmashauri hiyo kufanya jitihada za dharura kuhakikisha wanafunzi hao wanapata elimu kwa wakati.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime Vijijini ambaye pia ni Ofisa Mifugo na Uvuvi, Peter Nyanja, aliwaambia madiwani hao kuwa halmashauri yake ina upungufu wa madarasa 47. Hata hivyo, alisema ifikapo Februari wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa darasa la saba mwaka jana wataanza kidato cha kwanza.
Aliongeza kuwa katika mwaka huu wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba ni 5,367 na kati yao waliochaguliwa kwenda shule za bweni ni  15 huku waliochaguliwa kwenda shule mbalimbali za sekondari  za kutwa ni 3,293 na 2,055 walikosa kuchaguliwa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.
Mwenyekiti  wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji, Msitapha Masyani (Chadema), alisema halmashauri yake kupitia vikao mbalimbali inafanya jitihada za makusudi ili wanafunzi waliofaulu waende shuleni. 

KILIMANJARO

Mkoa wa Kilimanjaro unakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa zaidi ya 2,400 katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na ukosefu wa matundu ya vyoo 3,737.

Akitoa taarifa hiyo kwa MTANZANIA jana, Mkuu wa mkoa huo, Anna Mgwhira alisema shule za msingi zina upungufu wa vyumba vya madarasa 2,178 na sekondari 224.

Kwa shule za msingi alisema Wilaya ya Hai ina upungufu wa madarasa 308, Moshi Vijijini 283, Moshi Manispaa 272, Mwanga 164, Rombo 370, Same 572 na Siha 209.

Alisema shule za sekondari Wilaya ya Hai zina upungufu wa madarasa 29, Moshi Vijijini 72, Moshi Manispaa 6, Mwanga 59, Same 112 na Siha 18.

“Tuna changamoto ya upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari. Kwa sasa tumeweka mikakati ya kuhakikisha tunatatua suala hili kwa kujenga madarasa na pia nitoe wito kwa wananchi kushirikiana na Serikali katika ujenzi huo ili watoto wetu waweze kusoma,” alisema.

WAZIRI ATOLEA UFAFANUZI

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mwita Waitara, amesema Serikali imetoa siku tisini kwa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu wawe wameenda shule.

Akizungumza na vyombo vya habari jana, Waitara aliwataka wazazi ambao watoto wao wamefaulu, lakini wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kuvuta subira kwakuwa Serikali bado inaendelea na ujenzi wa madarasa.

“Tunaamini baada ya siku 90 wote watakwenda sekondari na watoto ambao wamechelewa watasoma kwa utaratibu maalumu ili waweze kuendana na wenzao ambao walishaanza masomo,” alisema Waitara.

Alisema shule ambazo zina walimu na madarasa kutakuwa na zamu kwa ajili ya kusomesha wanafunzi.

“Kila halmashauri ioneshe namna ambavyo itaendelea kujenga shule, kama kuna mkuu wa wilaya ama mkuu wa mkoa atakayeshindwa kumaliza ujenzi wa madarasa na kusababisha watoto wasiende shule wajue kabisa watakuwa wameshindwa kazi yenyewe,” alionya Waitara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles