WATU wengi hawafikirii mara mbili mbili kuhusu hisia za mguso au mpapaso. Mara nyingi hisia hizi hupuuzwa miongoni ukilinganisha na nyingine za fahamu.
Wanasaikolojia wanasema mguso una ‘miujiza’, nguvu za kipekee na manufaa mengi hasa kwa watoto wachanga, hivyo zinapaswa kupewa uzito kwa manufaa yao.
Kwa miaka mingi tu imekuwa ikifahamika kuwa mguso una nguvu kisaikolojia kwa watoto na watu wazima pia.
Nguvu ama manufaa hayo ni pamoja na kuimarisha mfumo wa kinga mwilini, kupunguza kiwango cha mapigo ya moyo, kuongeza mzunguko wa damu, kupunguza maumivu, shinikizo, wasiwasi, shaka na uchovu.
Hivyo basi, mguso ni mzuri kwa wanadamu. Na katika kuonesha namna gani ulivyo na manufaa, watoto wanaoukosa kibinadamu hasa mguso wa upendo wanaweza kujikuta wakikumbwa na mfadhaiko na hali ya wasiwasi, shaka na hata kushindwa kukua vizuri.
Kadhalika, mtoto anapokosa mguso, maendeleo ya makuzi ya watoto huchelewa na wana uwezekano mkubwa wa kuwa watu wa kulipuka kimachafuko, ghadhabu na tabia zisizokubalika katika jamii.
Mbaya zaidi, ukosefu wa mguso huu wa upendo, pia unaweza kusababisha kifo.
Wakati hilo likifahamika kwa miaka mingi, utafiti wa karibuni umebaini kuwa kumpapasa papasa mtoto au kumkanda taratibu kunapunguza kwa kiasi kikubwa shughuli katika ubongo wake hasa zinazohusiana na maumivu.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha John Moores cha Liverpool pia nchini humo, ulifuatilia shughuli za ubongo wa zaidi ya watoto 32, wakati walipokuwa wakitolewa na kupimwa damu.
Nusu yao walipapaswa papaswa na brashi nyororo iliyowekwa mkononi na walionyesha asilimia 40 ya kutokuwa na maumivu kwenye bongo zao.
Mwandishi wa vitabu Rebeccah Slater, anasema: Kumkanda kanda, kumshika au kumpapasa taratibu mtoto kuna nguvu na uwezo wa ajabu, na kwamba hakuna madhara ya pembeni kabisa.”
Utafiti huo pia umebaini kuwa, kasi ya kupunguza uchungu ni kama sentimita tatu kwa sekunde moja.
“Mara nyingi wazazi huwapapasa papasa watoto wao katika kasi ya kawaida tu,” anasema Profesa Slater.
“Ikiwa tutaelewa kinachofanyika ndani ya viungo vya mwanadamu hasa mawasiliano ya ubongo pamoja na mbinu za kupasha ujumbe wa kimya kimya ndani ya watoto, inawezekana kuboresha zaidi ushauri ambao huwa wanawapatiwa wazazi ili waweze kuwaliwaza watoto wao.”
Kitendo cha kumliwaza mtoto kwa kumpapasa papasa, huzindua aina fulani ya ‘niuroni’ iliyo na hisia katika ngozi iitwayo C-tactile afferents, ambayo inaonekana kupunguza maumivu kwa watu wazima.
Lakini matokeo ya utafiti hayakuweza kuonesha wazi, iwapo watoto wana mwitikio sawa au hukua kadiri muda unavyokwenda.
“Kuna ushahidi unaoonyesha kuwa, hisia iitwayo C-tactile afferents, inaweza kuzinduliwa ndani ya watoto, na mguso huo wa upole na taratibu, unaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye ubongo wa watoto hao,” anasema Profesa Slater.
Profesa Slater anasema utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Current Biology, na kuelezea ushahidi wa kina na wa nguvu ya mguso, uliopo chini ya mfuko wa kumbebea mtoto unaoitwa Kangaroo Care, mahali ambapo hutunza watoto waliozaliwa kabla ya muda.
Wazazi wanashauriwa kuwapa mguso, kupapasa au kuwakanda watoto wao katika harakati za kupunguza uchungu, wanayoweza kuyapitia hapo baadaye maishani.
“Kazi za awali zimeonyesha bayana kuwa mguso unaweza kuongeza uhusiano wa karibu kati ya mtoto na mzazi, kupunguza shinikizo la moyo kwa mama na mtoto na kupunguza muda mrefu wa kukaa hospitali kimatibabu au uangalizi maalumu,” anasema Profesa Slater.
Waandishi wa uchunguzi huo sasa wana mpango wa kurudia zoezi hilo kwa watoto waliozaliwa kabla ya muda wao (njiti), na ambao bado baadhi ya sehemu ya viungo vyao hasa sehemu zao za mwili zinazohusiana na kuhisi zinaendelea kukua.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Blissi, linalowashughulikia watoto wagonjwa nchini Uingereza, Caroline Lee-Dave, anasifia utafiti huo.
Aidha, utafiti wa mwaka 2017 ulibaini kuwa mguso kwa watoto wachanga huweza kuathiri kiwango cha chembe chembe za molecule na kutoa matokeo yenye manufaa ya kudumu kwa miaka mingi ijayo.
Utafiti huo uliochapishwa Novemba 22, 2017 katika Jarida la Development and Psychopathology, ulihusisha watoto wenye afya nzuri 94 huko British Columbia nchini Marekani.
Wazazi wenye watoto walio na umri wa miaka mitano walitakiwa kuandika katika vitabu vidogo vya matukio – yaani diary kuhusu tabia zao za kulala, kula, ubishi na kadhalika sambamba na ulezi unaohusisha kukutana na mguso wa mwili.
Ktika utafiti huo, wanasayansi walikuta matokeo tofauti baina ya mguso mkubwa na ule mdogo katika maeneo matano tofauti ya vinasaba (DNA).
Mawili kati ya maeneo hayo yaliangukia ndani ya vinasaba, moja likiwa na mchango katika mfumo wa kinga na lingine likihusika katika ‘metabolism’.
Watoto waliokuwa na afya dhaifu na kupokea kiwango kidogo cha mguso walikuwa na matatizo ya makuzi kulinganisha na wale wenye mguso wa kutosha pamoja na afya njema.
Aidha, utafiti ulioendeshwa na Chuo Kikuu cha California nchini Marekani ukihusisha wachezaji wa Ligi ya Mpira wa Kikapu wa NBA ulifichua sababu zinazopaswa kutiliwa mkazo, namna na kwa kiwango gani watu wanapaswa kugusana.
Matokeo ya utafiti huo yalionesha kiwango cha juu cha kugusana ikiwamo mgongoni baina ya wachezaji mwanzoni mwa msimu wa mashindano, wachezaji hao walikuwa na uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kipindi cha msimu mzima wa ushiriki wa ligi hiyo.
Ulionesha kwamba kugusana mara kwa mara kwa njia ya upendo na kutiana moyo, kunasaidia kujenga tabia ya kuaminiana na kushirikiana, hali ambayo moja kwa moja ilisababisha ufanisi katika michezo na timu.
Kwa sababu hiyo, tabia hiyo ikihamishiwa kwa watoto inaweza kuleta mafanikio kwa familia na hata jamii kwa ujumla