SAFINA SARWATT-MOSHI
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania bara, Rodrick Mpogolo alisema mwishoni mwa wiki kuwa tamaa ya rushwa na migogoro baina ya viongozi wa chama hicho imechangia kushindwa kulikomboa Jimbo la Moshi Mjini kwa miaka 30.
Mpogolo aliyasema hayo wakati akifungua semina ya mafunzo ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijijini na vitongoji kwa wajumbe wa halmashauri kuu na mabalozi wa CCM, Manispaa ya Moshi.
Mpogolo alisema CCM Moshi Manispaa haina budi kujitafakari katika maeneo yote pale waliposhindwa katika uchaguzi uliopita na kuzifanyia kazi kasoro hizo ili uchaguzi ujao ya Serikali za mitaa, waweze kuzikomboa kutoka upinzani.
Mpogolo alisema uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji mwaka huu ndio msingi wa kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 huku akitoa wito kwa viongozi na wanachama kushikamana na kuwa imara muda wowote.
“Kila shina na matawi ya CCM lazima wajifanyie tathimini ya kutosha na kuangalia nani anayefaa na anakubalika ndani ya chama na katika jamii na ushiriki wake katika shughuli za ujenzi wa taifa ili wananchi waweze kuchagua kiongozi safi.
“Maeneo mengi wagombea wa CCM wamekuwa wakishindwa katika uchaguzi kutokana na kutokukubalika katika jamii na hivyo kupoteza kata na hata jimbo,”alisema.
Aidha Mpogoro katika ziara hiyo alitoa wito kwa mabalozi, wenyeviti wote wa CCM kukagua majina, kuongeza idadi ya wanachama katika mashina yao kwani kila balozi anatakiwa kuwa na wajumbe wasiopungua 50 na kuendelea.
Awali Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi akimkaribisha Mpogolo alisema chama kimejiandaa vizuri kukomboa kata na majimbo yote yaliyopo upinzani.
Alisema wakazi wa mkoa huo hawapo tayari kurudia makosa ya uchaguzi mkuu uliopita na wameona utekelezaji wa ilani ya CCM chini ya Rais John Magufuli katika nyanja mbalimbali inavyotekelezwa.