Mohamed Hamad, Simanjiro
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,William Ole Nasha, amesema jamii ya kifugaji itaondokana na changamoto za migogoro ya ardhi endapo itapeleka watoto wao shule.
Ole Nasha amesema hayo wakati akiongea na wazazi, walimu na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kitwai A, iliyopo wilayani Simanjiro ambayo ilijisahihisha kwa kufanya vizuri mtihani wa darasa la saba kitaifa baada ya kufanya vibaya mwaka jana.
“Nimeambiwa watoto watakaojiunga na darasa lakwanza Januari mwakani ni 49, hii si kweli mna watoto wengi kulingana na idadi yenu, nataka kupata ripoti kamili kuhusu ongezeko la wanafunzi kujiandikisha hapa shuleni,” amesema.
Pamoja na mambo mengine wamewataka Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Yefred Myenzi, kuendeleza jitihada walizoanza za kuinua elimu shuleni kwa kuongeza idadi ya wanafunzi watakaoanza darasa la kwanza huku akiahidi kujenga madarasa mawili.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, James Ole Millya (CCM), aliahidi kuchangia mifuko 250 ya saruji akisema alisoma shule hiyo tena chini ya miti kwa kutokuwa na madarasa.