26.1 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Vitambi vyawatesa wanawake

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM



WANAWAKE ndilo kundi linaloonekana kuathiriwa zaidi na uzito uliokithiri pamoja na kiribatumbo (kitambi) ikilinganishwa na wanaume, nchini imeelezwa.

Tatizo la uzito uliokithiri kwa watu wazima ni asilimia 26, huku wanawake wakiwa ni waathirika zaidi kwa asilimia 37  ikilinganishwa na wanaume wenye asilimia 15.

Kwa upande wa kiribatumbo wanawake wanaongoza kwa kiwango cha asilimia 15 na wanaume asilimia 2.5.

Hayo yalielezwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Uzito Uliozidi na Kiribatumbo Duniani ambayo hufanyika Novemba 26, kila mwaka.

Alisema takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti wa ‘Step Survey’ uliofanyika nchini 2012 na kwamba bado kuna ongezeko la tatizo la unene uliozidi na kiribatumbo (obesity).

Dk. Ulisubisya alisema nchi zenye kipato cha kati na chini Tanzania ikiwamo huathirika zaidi na matatizo hayo.

“Magonjwa yasiyo ya kuambikiza ni pamoja na kisukari, saratani, moyo, na yale ya hewa ambayo tunakabiliana nayo hivi sasa na kwa bahati mbaya mno bado tunakabiliwa pia na magonjwa ya kuambukiza kama vile kuhara, nimonia, malaria, kifua kikuu na Ukimwi,” alisema.

Alisema matatizo ya uzito uliokithiri na kiribatumbo yapo kwa kasi kubwa katika maeneo ya mijini kuliko vijijini.

“Kwa sababu watu wengi wanaohamia mijini hubadili mtindo wa ulaji bora unaochangia kutunza afya na kuzuia kuongezeka kwa uzito wa mwili,” alisema.

Dk. Ulisubisya alisisitiza ulaji wa vyakula vya asili vya kupikwa kwa njia ya asili kama vile mihogo, viazi na magimbi ya kuchemsha, mboga za majani na matunda ya asili, ili kuzuia ongezeko la mwili na vitambi.

“Kunywa vinywaji visivyo na sukari nyingi matumizi kidogo ya chumvi na mafuta, kufanya kazi za kutumia nguvu na kutembea kwa muda mrefu, kitendo cha watu kuhamia mijini kimebadili tabia za wengi,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles