31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 5, 2024

Contact us: [email protected]

Lugola asisitiza uimara wa jeshi la polisi

Na Mwandishi Wetu- Mwibara



WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Jeshi la Polisi lipo imara kupambana na uhalifu wa aina yoyote utakaojitokeza nchini hivyo wahalifu wasithubutu kulichezea wala ‘kulibipu’.

Lugola pia amewataka wananchi kuendelea kuwapa taarifa za uhalifu Polisi ili ziweze kufanyiwa kazi haraka.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Ragati, Kata ya Kasuguti, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, Lugola alisema jeshi hilo litaendelea kuwalinda wananchi na mali zao lakini  ili waweze kufanya hivyo, wananchi wanapaswa kuwasaidia kufichua uhalifu katika maeneo wanayoishi.

Lugola aliyazungumza hayo baada ya wananchi wa kijiji hicho kusema kuna kundi la vijana ambalo linaongozwa mwananchi mmoja kijijini hapo, linahatarisha amani na kuwafanya kuishi kwa wasiwasi.

“Polisi wapo kwa ajili yenu, kuweni huru muda wowote kutoa taarifa za kiuhalifu katika maeneo yenu, kutokana na viashiria hivyo vya uvunjifu wa amani katika kata hii namuagiza mkuu wa polisi wilaya (OCD) kuwasaka, kuwakamata wale wote ambao wanahatarisha amani katika kata hii ya Kasuguti,” alisema Lugola.

Lugola aliwaeleza wananchi wa kata hiyo iliyo kwenye Jimbo lake la Mwibara kuwa waendelee kufanya shughuli za maendeleo na pia waanze maandalizi ya kilimo naye atahakikisha anatoa misaada mbalimbali ikiwemo mbegu ili waweze kupata mazao yaliyo bora kwa hapo baadaye.

Kuhusu vitambulisho vya taifa, Lugola alisema vitatolewa kwa Watanzania wenye sifa na haki yao kupata lakini ili waweze kupata vitambulisho hivyo lazima wapitie katika mchujo ili kuepusha kutoa kwa wasio raia.

Alisema mchujo huo unaofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) upo makini ili kuhakikisha hakuna makosa yatakayofanywa wakati wa utoaji wa vitambulisho, hivyo wananchi wawe na uvumilivu wakati mchujo huo ukiendelea.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles