25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Tunatarajia mengi JKCI

TAARIFA ya wiki hii iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi, inatia matumaini baada ya kusema kuwa wamebakiza hatua chache kabla ya kuanza kufikia ndoto yao ya kupandikiza moyo nchini.

Katika hilo, Profesa Janabi alisema wamedhamiria kufikia hatua ya kufanya upasuaji huo mkubwa ambao haujawahi kufanyika nchini kwa kuwatibu watu wenye matatizo ya moyo.

Alisema kuna matarajio makubwa, kwani tangu taasisi hiyo ilipoanzishwa mwaka 2015, umefanyika upasuaji wa kibigwa wa aina mbalimbali kutibu magonjwa ya moyo kwa mafanikio makubwa.

Miongoni mwa upasuaji ambao alisema unawapa nguvu ya kufanya vizuri zaidi siku zijazo ni kuvuna mishipa ya damu kutoka miguuni na kuipandikiza katika moyo ili kuizibua iliyoziba kwa mtu mzima mwenye umri wa miaka 82.

Mwingine ni ule uliofanyika hivi karibuni wa kuzibua mishipa ya moyo ya mtoto mdogo wa wiki mbili iliyokuwa imeziba.

Kwamba tangu mwaka 2015 hadi sasa, wagonjwa 200,000 wamepatiwa matibabu katika Taasisi hiyo na ikiwa wangepelekwa nje ya nchi ingechukua miaka 14 kufikia idadi hiyo.

Sisi MTANZANIA Jumapili tunadhani juhudi hizi za JKCI zinapaswa kuungwa mkono na tuna imani wananchi waliofikishwa hospitalini hapo na kupatiwa matibabu pengine ingewachukua muda mrefu kukamilisha taratibu za kupelekwa nje ya nchi na huenda wapo ambao wangepoteza maisha kutokana na kusubiri.

Mbali na JKCI kusaidia kuokoa fedha nyingi za Serikali ambazo zingetumika kuwasafirisha wagonjwa pamoja na kugharamia matibabu yao wakiwa katika hospitali nyingine huko nje ya nchi, lakini ukweli ni kwamba imekuwa msaada kwa baadhi pamoja na kuwapo kwa changamoto.

Tunatarajia kuona mengi zaidi yakifanyika katika Taasisi ya JKCI, ambayo imekuwa kimbilio la wananchi wengi hapa nchini.

Pamoja na taasisi hiyo kupokea wagonjwa wa rufaa kutoka nchi za Uganda, Kenya, Malawi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini tuna imani kwa matibabu hayo na uwezo mkubwa wa kufanya upasuaji wa moyo pamoja na taratibu za kupandikiza zitakapoanza kutafungua wigo mpana zaidi kwa watu kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini kupatiwa matibabu yaliyo bora zaidi.

Sisi MTANZANIA Jumapili tunaitaka Taasisi hiyo kutorudi nyuma na kujikita katika tafiti na uchunguzi mkubwa zaidi ili kugundua mbinu nyingine bora zaidi za kutoa matibabu kwa wagonjwa wa moyo.

Tuna imani kubwa na jitihada zinazofanywa na Taasisi hiyo kupitia madaktari wake bingwa katika kuhakikisha matibabu ya wagonjwa hao yanakuwa bora na yenye ufanisi.

Pia tunasisitiza Watanzania kujijengea utaratibu wa kula mlo kamili na kuepuka kula hovyo, kufanya mazoezi pamoja na kujiwekea utaratibu mzuri wa maisha yao ya kila siku ili kutokuwa chanzo cha magonjwa, ikiwamo yale moyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles