MFALME Salman wa Saudi Arabia ameiwekea vikwazo kampuni yenye ushawishi mkubwa nchini humo ya Binladen Group.
Kampuni hiyo inamilikiwa na familia ya kiongozi wa zamani wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, Osama bin Laden. Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kuanguka kwa winchi katika msikiti mkubwa mjini Mecca, iliyowaua watu 107 na kujeruhi wengine karibu 400 siku chache kabla ya ibada ya hija.
Kamati ya Uchunguzi imeona kuwa kampuni hiyo imebeba dhamana kwa janga hilo lililotokea Ijumaa iliyopita wakati mvua kubwa iliyoandamana na upepo mkali iliposababisha ajali hiyo. Shirika la Habari la Serikali (SPA) limesema wachunguzi wamegundua winchi hiyo haikuwa mahala ilipotakiwa kwa sababu mkono wake mrefu ulitakiwa uwe umeteremshwa.
Wakuu wa kampuni hiyo, wamezuiwa kusafiri nje ya nchi hadi mchakato wa kisheria utakapokamilika. Mfalme Salman amewaamuru waendesha mashtaka wawafungulie mashtaka wakuu hao.