CAPENHAGEBN-COPENHAGEN, DENMARK
SERIKALI ya Denmark imeamua kutoipatia silaha na vifaa vya jeshi Saudi Arabia kutokana na tukio la kuuawa mwandishi habari mkosoaji wa ufalme huo, Jamal Khashoggi.
Mbali ya mauaji hayo yaliyotokea katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia nchini Uturuki, Denmark imeeleza kuchukizwa na ushiriki wa nchi hiyo katika vita vya Yemen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Enders Samuelsen alisema: “ Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya nchini Yemen na kuuawa kwa Khashoggi imebidi tuchukue hatua.”
Kabla ya hapo, Ujerumani pia ilipitisha uamuzi kama huo na kuamua kusimamisha moja kwa moja biashara ya silaha pamoja na Saudi Arabia huku Ufaransa ikisema itaamua hivi karibuni kuiwekea vikwazo.
Saudi Arabia, ambayo ni mnunuzi mkubwa wa silaha duniani inaongoza jeshi la ushirika wa Kiarabu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Yemen ambako maelfu ya watu wameuawa na kusababisha maafa makubwa kwa raia.