Elizabeth Joachim, Dar es Salaam
Wazazi mkoani Tabora wametakiwa kuwapa elimu ya uzazi watoto wao wa kike wenye umri chini ya miaka 18, pindi wanavyopevuka ili kuwasaidia kuepukana na mimba za utotoni.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Idara ya Mradi wa mapambano dhidi ya mimba za utotoni  Dar es salaam  (MAE), Chance Ezekiel,   leo Jumatatu Novemba 19 na kuongeza kuwa baadhi ya wazazi wamezikumbatia mila na desturi kwa kuamini mama pekee ndiye ana uwezo wa kumlea mtoto wa kike.
“Mradi huu umepita katika mikoa mitatu na hapa Tabora ndipo tunapohitimisha baada ya kutoka Shinyanga, Mkoa wa Dar es salaam ndiyo mkoa tuliozindulia mradi huu.
“Nitoe wito kwa wakazi wa Tabora kujitokeza kwa wingi ili muweze kuelimika na kujua madhara ya mimba za utotoni,’’ amesema Ezekiel.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi huo, Edgar Chatanda, amesema wameamua kutoa elimu ya mapambano dhidi ya mimba za utotoni kwa njia ya sanaa wakiamini sanaa ni burudani ina uwezo wa kuteka watu wengi kwa wakati mmoja.