33.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wanariadha hawa wamerudisha nuru ya mbio Tanzania

NA JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM



MCHEZO wa riadha ni miongoni mwa michezo iliyowahi kuliletea sifa Tanzania miaka ya nyuma, hususan enzi za akina Filbert Bayi na Suleiman Nyambui ambao rekodi zao zimewea kudumu zaidi ya miaka 35.

Mategemeo na akili za wadau wa mchezo wa riadha kwa sasa ni mashindano ya Olimpiki ambayo yanatarajiwa kufanyika mwaka 2020 jijini Tokyo, Japan.

Ikiwa bado mwaka mmoja wa maandalizi kabla ya mchakamchaka wa mashindani hayo kuanza, Tanzania imeanza kuonyesha taswira nzuri kupitia wanariadha wake walioweza kushiriki mbio tofauti za kimataifa ndani ya mwaka huu.

2018 umekuwa mwaka wa kipekee kwa mchezo wa riadha hapa nchini, hii ni kutokana na juhudi ambazo zimeweza kuonyeshwa na wanariadha mbalimbali waliopata nafasi ya kuliwakilisha taifa katika mashindano tofauti.

Tofauti na miaka ya nyuma pindi tunapokabiliwa na mashindano makubwa ya kimataifa, tayari taswira ya anguko la Tanzania katika mashindano hayo upande wa mchezo huu, huanza kujulikana mapema.

Hadi sasa tayari Tanzania inauwezo wa kusimama kifua mbele na kujinadi kumiliki wanariadha wazuri wanaoweza kuleta upinzani mkali katika mashindano yoyote ya kimataifa.

SPOTIKIKI inakuletea orodha ya wanariadha ambao wameweza kuonyesha nia ya kupokea vijiti walivoviacha Nyambui na Bayi. Huku vipaji vipya kama Marco Joseph, Amina Mohamed, Rosalia Fabian, Silvia Masatu na Wilbert Peter vikianza kuonyesha makali.

Rekodi zao zinawabeba

Felix Simbu

Alianza kuwika na kutambulika ulimwengu wa riadha dunaini, baada ya kushika nafasi ya kwanza katika mbio za Standard Chartered Marathon huko nchini India. Akiwa ametumia muda wa saa 2:09:32 aliweza kutangazwa mshindi.

Mwanzo huo mzuri ulimwezesha kufungua milango ya mafanikio, ambapo nguvu zote alizihamishia kwenye mashindano ya Olimpiki zilizofanyika jijini Rio nchini Brazil na kufanikiwa kushika nafasi ya tano mbio za marathon.

Mbali na mbio hizo, Simbu ameweza kujijenga uzoefu na umaarufu kupitia mashindano mengine yaliyotambulika kama IAAF World Championships zilizofanyika mwaka jana jijini London, England na kushika nafasi ya tatu.

Mwaka huu kule nchini Colombia, Simbu alishiriki mbio za Bogota International Half Marathon lakini alishindwa kumaliza kutokana na kile kinachodaiwa majeruhi lakini anabaki kuwa tegemeo na mwangaza wa Tanzania mashindano ya Tokyo 2020.

Augistino Sulle

Moja ya mafanikio yake ni kuvunja rekodi ya mbio za marathon nchini iliyowekwa na mkongwe Juma Ikangaa mwaka 1989.

Sulle alishiriki mbio za Toronto Marathon huko nchini Canada na kuweka muda bora wa saa 2:07:44.

Kiwango cha mwanariadha huyu kutoka Klabu ya Talent jijini kinazidi kuimarika na amekuwa akitoa upinzani kwa Alphonce Felix Simbu.

Fabian Joseph

Ubora wake ulizidi kuimarika zaidi pindi alipofanikiwa kufanya vema katika mashindano ya Ngorongoro Marathon. Kupitia mbio hizo, aliweza kujiwekea rekodi ya kuibuka mshindi kwa kumaliza ndani ya saa 1:03:47.

Joseph ni miongoni mwa wanariadha wenye uzoefu wa kushiriki mashindani mengi ya kimataifa, licha ya kushindwa kutwaa medali.

Lakini kupitia mbio za zilizofanyika hivi karibuni za Nagai Marathon nchini Japan, ameweza kujiongezea ubora kwa kutwaa medali ya dhahabu, upande wa mbio fupi.

Emmanuel Giniki

Ubora wa rekodi yake ulinogeshwa na ushindi wa Shanghai China, alifanikiwa kuibuka wa kwanza kubeba medali ya dhahabu, baada ya kumaliza mbio hizo za nusu Marathon ndani ya  dakika 01:01:36.

Giniki hivi karibuni alifanikiwa kumaliza nafasi ya pili katika mbio za kilomita 10 nchini Uholanzi na kupatiwa medali ya fedha, huku akiwa ametumia muda wa dakika 27:37.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles