Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Mbunge wa Jimbo la Ukonga ambaye pia Naibu Waziri Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara ametangaza oparesheni ya kuhakikisha wanafunzi wanaandikishwa shule na watakaowakwamisha suala hili kwa ajili ya michango kukiona.
Waitara amesema hayo jana jioni katika Kata ya Chanika alipokuwa na mkutano wa kuwashukuru wananchi wa jimbo lake kwa kumchagua.
“Nasimamia kwa karibu suala la elimu, michango yenye kero imeondolewa, watoto darasa la awali, la kwanza na kidato cha kwanza waandikishwe, hii ni oparesheni ya kuhakikisha wanaandikishwa.
“Ni marufuku kuzuia mwanafunzi kujiunga darasa la awali, la kwanza na kidato cha kwanza kama mzazi wake hajatoa michango, ukizuiliwa kuandikisha mtoto sababu hujatoa mchango toa taarifa,” amesema Waitara.
Amesema Serikali inakataza michango yenye kero hivyo atakayezuia watoto kuandikishwa kwa sababu hiyo atachukuliwa hatua.