BRUSSELS, UBELGIJI
MKUU wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ameiambia wazi Saudi Arabia kwamba bado inahitajika kutoa ufafanuzi kamili juu ya kile alichokitaja kuwa uhalifu mbaya.
Hilo limekuja licha ya waendesha mashitaka wa Saudi Arabia kuelekeza lawama kwa watuhumiwa watano kuwa ndio waliomuua mwandishi Jamal Khashoggi katika ubalozi wa Saudia nchini Uturuki.
Juzi, Rais Donald Trump wa Marekani alisema kwamba ripoti zilizosema serikali yake imefikia hitimisho hazikuwa sahihi.
Aliwaambia wanahabari alipokuwa akienda California kuangalia athari za moto kwamba atapata taarifa kamili leo au kesho na kuwa Saudi Arabia ilikuwa mshirika mzuri.
Siku ya Ijumaa gazeti la Washington Post la Marekani na Shirika la Habari la Associated Press yaliripoti kuwa Shirika la Ujasusi Marekani (CIA) limehitimisha kuwa mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman aliagiza kuuawa kwa Khashoggi madai ambayo awali yalikanwa na Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Saudi Arabia Shalann al-Shalaan.