32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Majaliwa aishukuru China kwa kutoa mikopo ya gharama nafuu

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameishukuru Serikali ya China kwa kuunga mkono jitihada za maendeleo zinazofanyika nchini hivi sasa kwa kutoa misaada ya mikopo ya gharama nafuu.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa juzi jioni alipokutana na Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Watu wa China, Cai Dafeng.

“Tunaishukuru Serikali ya China kwa sababu tumepokea misaada na mikopo ya gharama nafuu na kuendeleza miradi mbalimbali kama vile mradi wa umeme wa Kinyerezi, awamu ya pili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Zanzibar,” alisema.

Alisema Serikali ya China imekuwa pia na uhusiano wa muda mrefu na Serikali ya Tanzania na hasa katika sekta ya afya ambapo kuna wanafunzi wengi wa Kitanzania wako nchini humo wakisomea udaktari na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

“Tuna uhusiano mzuri katika sekta ya afya na sasa hivi tuna madaktari 20 ambao wanasoma huko na wengine wanasomea masuala ya Tehama. Pia tuna uhusiano mzuri baina ya Bunge la Tanzania na China,” alisema.

Pia alisema Tanzania imejipanga kuinua uchumi wake kupitia ujenzi wa viwanda na sekta nyingine kama utalii kutokana na vivutio vilivyopo nchini.

“Nimefurahi kusikia kuwa hivi karibuni tutapata idadi kubwa ya watalii kutoka China,” alisema.

Kwa upande wake, Dafeng, alisema amefurahishwa na jinsi Serikali inavyoendelea kubadili hali ya uchumi wa nchi na maisha ya Watanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.

Alisema China itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika masuala ya kiuchumi na haiko tayari kuona ikiingiliwa masuala yake ya ndani na mataifa kutoka nje.

Kuhusu masuala ya uwekezaji baina ya Tanzania na China, alisema itaendelea kuzihimiza kampuni za nchi hiyo ziwekeze hapa nchini katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.

“China inatarajia kuongeza uwekezaji kwenye kilimo, nishati na miundombinu,” alisema.

Kuhusu elimu, alisema Serikali ya nchi hiyo inaangalia uwezekano wa kuanzisha masomo ya lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ili Watanzania wengi zaidi wajifunze na kuhusu afya, alisema wataendelea kutuma madaktari wake ili waje kutoa huduma kwa Watanzania na inatamani kuona uhusiano baina ya mtu mmoja mmoja kutoka nchi hizo mbili ukiendelea kukua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles