30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Kibano vyama vya siasa

Na Fredy Azzah-Dodoma

MUSWADA wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa kwa Mwaka 2018 umesomwa bungeni kwa mara ya kwanza jana, ambako pamoja na mambo mengine, umeainisha maeneo 10 yatakayokuwa msumari kwa vyama vya siasa, hususan vile vya upinzani nchini.

Kwa mujibu wa muswada huo, mtu ama taasisi iliyosajiliwa nchini au nje ya nchi, ikitaka kutoa elimu ya uraia ama kujengea uwezo kwa vyama vya siasa, lazima iandike taarifa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kueleza madhumuni ya mafunzo, ratiba ya mafunzo, watu wanaohusika kwenye hayo mafunzo, vifaa vya mafunzo na matokeo yanayotarajiwa kutokana na mafunzo hayo.

“Msajili anaweza kukataa mafunzo hayo na kutoa sababu, atakayekiuka kifungu hicho anaweza kutozwa faini ya Sh milioni moja hadi tano ama kifungo cha miezi sita hadi 12,” unaeleza muswada huo.

Unasema pia, chini ya sheria hiyo, hakuna shitaka litakalofunguliwa dhidi ya Msajili, Msajili Msaidizi, Mkurugenzi au ofisa yeyote kwenye wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa jambo lolote lililofanywa ama kukatazwa kufanywa kwa nia njema.

Muswada huo pia unakataza vyama vya siasa kuanzisha vikundi vya ulinzi kutoa mafunzo ya aina yoyote ya kijeshi, kiulinzi au yanayofanana na hayo.

Kuhusu vyama vya siasa kuungana, Muswada huo unapendekeza jambo hilo lazima likubaliwe na mkutano mkuu wa vyama vilivyoamua kuungana.

Baada ya suala hilo kupitishwa na vyama, Msajili wa Vyama vya Siasa atafuta vyama vilivyoungana na kusajili chama kipya kwa jina lililopendekezwa.

Kuhusu ruzuku za vyama, muswada huo unampa msajili mamlaka ya kuzuia ruzuku kwa chama cha siasa kwa muda unaojulikana au usiojulikana pale atakapoamini kuwa uongozi wa chama cha siasa pamoja na bodi yake ya wadhamini haifanyi matumizi mazuri ya fedha hizo.

Msajili wa Vyama vya Siasa pia anapewa mamlaka ya kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi kwenye chama husika pale anapoona mambo hayako sawa.

Vyama pia vinapaswa kuteua maofisa masuhuli ambao watakuwa na jukumu la kusimamia mali za chama husika.

Muswada huo pia umeongeza vigezo anavyopaswa kuwa navyo mtu anayegombea nafasi ya uongozi kwenye chama cha siasa.

“Lengo la marekebisho haya ni kuzuia watu waliofilisiwa na wale wasio na vigezo na kushika nafasi katika ofisi za umma kugombea uongozi kwenye vyama vya siasa,” unasema Muswada huo.

Pia kwa mujibu wa Muswada huo, vyama vya siasa vitatakiwa kuwasilisha kwa msajili tamko la mapato yake yote na matumizi.

Pia muswada huo unapiga marufuku uanzishwaji wa vikundi vya kisiasa kwenye shule, vyuo, maofisi na maeneo ya dini.

Vyama pia vinapigwa marufuku kujihusisha na shughuli zozote zenye mwelekeo wa kiharakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles