32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Spika: Hawa ndio mawaziri, wabunge vinara kwa utoro bungeni

Na Fredy Azzah -Dodoma

 

SPIKA wa Bunge Job Ndugai, amesema Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga, ndio vinara wa utoro katika vikao vya Bunge.

Ndugai alisema mahudhurio ya wabunge hao yamechukuliwa kutoka katika vikao vya kamati za Bunge 33 ambavyo vilikaa Machi, Agosti na Oktoba na vikao 61 vya mkutano wa 11 wa Bunge la Bajeti na tisa vya Bunge la 12.

Alisema taarifa hiyo aliyoitoa bungeni jana, siyo ya kisiasa kwa sababu mahudhurio hayo ni kwa mujibu wa usajili ambao wabunge hufanya kwa njia ya kielektroniki mara waingiapo katika vikao.

 

MAWAZIRI WATORO

Ndugai aliwataja mawaziri waliopata alama chache katika mahudhurio hayo na asilimia zao katika mabano kuwa ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina (45) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (41).

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi (38), Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba (37) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahiga (35).

“Mahudhurio yao si mazuri, lakini waziri ambaye ana mahudhurio mazuri amepata asilimia 90, ambaye ni Jenista Mhagama (Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), wengine wote wanasuasua tu,” alisema Ndugai.

Alisema suala la utoro si zuri na mawaziri wakati wa Bunge wanapaswa kuhudhuria vikao na kama hawapo watoe taarifa.

 

MANAIBU WAZIRI WAHUDHURIAJI

Ndugai alisema kwa upande wa manaibu waziri, mwenye mahudhurio mazuri zaidi ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, ambaye amehudhuria vikao vyote vya kamati na vya Bunge.

Wanaomfuatia ni Hamad Masauni (Wizara ya Mambo ya Ndani), Antony Mavunde (Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) na Mussa Sima (Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano).

Wengine ni Abdallah Ulega (Wizara ya Mifugo na Uvuvi), John Kuandikwa (Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi) na Atashasta Ndetye (Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi).

 

WABUNGE WATORO

Ndugai aliwataja wabunge wenye mahudhurio mabaya kuwa ni Salim Hamis Salim (Meatu – CCM), Mansour Yusuph Himid (Kwimba – CCM), Abdul Azizi (Morogoro – CCM), Hussen Nassoro Amar (Nyangwale – CCM), Mbaraka Bawazir (Kilosa – CCM) na Dk. Mathayo David (Same Magharibi – CCM).

Wengine ni John Mnyika (Kibamba – Chadema), Salim Hassan Turky (Mpendae – CCM), Suleiman Nchambi (Kishapu – CCM) na Mbunge wa Arusha Mjini, Lema (Chadema) anayeongoza kwa mahudhurio mabaya akihudhuria vikao vya kamati na Bunge kwa asilimia 7.8 tu.

“Na hii si habari njema kwa wapigakura wenu ambao mnategemea kusimama tena kuwaongoza wakati mahudhurio yenu ni haya. Na pia mahudhurio yenu haya nayapeleka kwenye vyama vyenu nao wajue maana tumeshasema sana,” alisema.

 

WABUNGE WALIOHUDHURIA KWA 100%

Ndugai aliwataja wabunge waliohudhuria vikao vyote kwa asilimia 100 ni Justin Monko (Singida Kaskazini), Felister Bura (Viti Maalumu) na Omary Kigua (Kilindi) ambao wote ni wa CCM.

Wanaofuatia ni Joel Mwaka (Chilonwa – CCM), Halima Bulembo (Viti Maalumu – CCM), Mbarouk Salim Ali (Wete – CUF), Hawa Mchafu (Viti Maalumu – CCM), Allan Kiula (Iramba Mashariki – CCM), Rashid Shangazi (Lushoto – CCM) na Mendard Kigola (Mufindi Kusini – CCM).

Wengine ni Augustine Masele (Mbogwe – CCM), Innocent Bashungwa (Kerwa – CCM) na Juma Hamad Omary (Ole – CUF)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles