Na ANDREW MSECHU – dar es salaam
MKURUGENZI Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema hoja ya Katiba mpya haiwezi kufa.
Amesema juhudi za kuipata zinatakiwa kwa kuwa ndiyo inayoweza kujenga taifa la ustaarabu.
Butiku alikuwa akizungumza wakati wa kumbukizi ya miaka mitano ya aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Katiba, marehemu Dk. Sengondo Mvungi, Dar es Salaam jana.
Alisema ingawa hoja ya Rais Dk. John Magufuli kuwa Serikali yake haina fedha za kutengeneza Katiba mpya inatakiwa kueleweka, suala hilo bado haliepukiki.
“Hoja kubwa ya Rais Magufuli ni kwamba suala la Katiba halikuwa agenda yake katika kampeni yake mwaka 2015.
“Anajua Watanzania wanaihitaji, hana hela ya kulipia ubishani wa Katiba… hii ni agenda ya Watanzania. Maadamu Watanzania wanaishi, mijadala ya Katiba mpya haiwezi kwisha,” alisema.
Alisema ingawa Rais anaona fedha hizo haziwezi kutoka katika kodi inayotumika kujenga miundombinu na kulipia elimu, inabidi ufanyike mkakati maalumu hata ikibidi kuwaomba Watanzania walipe kodi maalumu kwa Katiba Mpya, kwa kuwa ni agenda yao inayoishi.
Butiku alisema analazimika kulisema hilo kwa kutumia uzee wake ingawa anajua kuzungumzia mambo aliyosema Rais kama alivyozungumza katika Kongamano la Hali ya Uchumi na Siasa lililoandaliwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Novemba 2, mwaka huu ambayo hayako katika maandishi kama alivyosikia si suala jepesi.
Hata hivyo alisema la msingi ni kwamba Rais anatambua Watanzania wanahitaji Katiba na hajazuia mjadala huo.
Alisema Katiba iliyopo haikidhi mahitaji ya sasa kwa kuwa hata Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere aliwahi kusema alifikiria namna ya kupunguza madaraka makubwa ya Rais ambayo yanaweza kumfanya kuwa dikteta, suala ambalo linaweza kubadilishwa iwapo itapatikana Katiba Mpya.
“Ninashauri katika uzee wangu tuendelee kuzungumza na kushauriana, tumwombe Mungu tupate Katiba Mpya kwa sababu Katiba ndiyo inayojenga misingi ya kuendesha taifa. Ndani ya Katiba ndiyo kuna sheria mama zinazotumika kutawala hulka za watu,” alisema.
Alisema Watanzania wanahitaji Katiba itakayosaidia namna ya kuishi kama watu huru wanaojitegemea.
Butiku alisema hata juhudi za Rais kupambana na wawekezaji ambao ana shaka nao kwa nia ya kutaka taifa lijitegemee, hazitawezekana kama hakuna Katiba huru.
Akimzungumzia marehemu Dk. Mvungi, alisema alikuwa mtu huru aliyekuwa akipumua Katiba na hata sasa bado msimamo wake na fikra zake kuhusu Katiba Mpya bado zinaishi, akiwa mjumbe aliyekuwa katika kamati ngumu iliyokuwa ikichukua maoni kuhusu Muungano.