30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi Songwe wamkataa DC, wamuomba RC aondoke naye

NA IBRAHIM YASSIN- SONGWE

WAKAZI wa Songwe mkoani Songwe wamemshitaki Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah, kwa Mkuu wa Mkoa huo, Brigedia Jenerali Nicodemas Mwangela, wakimtuhumu kwa utendaji mbovu, ikiwamo kujihusisha na ujasiriamali na ameshindwa kuwatumikia.

Wakazi hao walitoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara na kusababisha Mwangela kufanya ziara kutembelea maeneo yanayolalamikiwa na kujionea jinsi wilaya hiyo ilivyokuwa na changamoto.

Katika mkutano huo uliofanyika juzi, wakazi wa wilaya hiyo walimueleza Mwangela kuwa DC wao ni mzigo, anawaongoza kwa ubabe, huku akishindwa kuwatumikia pamoja na kumhusisha katika shughuli za ujasiriamali kupitia wawekezaji na kuchoma moto nyumba za wananchi.

Mkazi wa Mkwajuni, Mdangala Dominiki, alisema wilaya hiyo haina mkuu wa wilaya, kwa sababu ameshindwa kusimamia fedha za wanawake na vijana kwa kuweka masharti mengi ambayo wana vikundi wanashindwa kutimiza, huku fedha hizo wanakopeshana viongozi wenyewe.

Naye Sebans Ngonja, mkazi wa Songwe, alisema kuna utoroshwaji wa mawe ya madini kutoka wilaya hiyo kwenda nyingine na wawekezaji wakikamatwa katika kizuizi wanatoa maneno ya kejeli, huku wakisema wamemalizana na DC.

“Kila lori linapokamatwa likibeba mkaa, magogo na mbao walinzi wa getini wanaambiwa ni mali ya Mkuu wa Wilaya na ukienda sehemu za uchimbaji maeneo yenye dhahabu unaambiwa makarasha ni yake, hivi amekuja huku kutumia cheo chake kufanya biashara,” alihoji.

Pia alisema baada ya kusikia Rais Dk. John Magufuli atafanya ziara wilayani humo kuna baadhi ya vitu ameficha katika nyumba za watu ili asibainike.

Baada ya wananchi kuzungumza kero zao, Mwangela alimkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Abraham Sambila, kuzungumza nao na wananchi walimshangilia, tofauti na DC aliyekuwa akizomewa kila mara na kusababisha kushindwa kujibu tuhuma hizo.

 

Sambila alimueleza Mwangela kuwa hoja za wananchi zipo sawa, akidai kuna ubabaishaji wa kiutawala katika Ofisi ya DC, hasa katika utoaji wa fedha za mkopo kwa wanawake na vijana na kutokana na masharti magumu pasipo kujali ufukara walionao wananchi.

Akijibu hoja za wananchi hao, Mwangela alisema amezichukua tuhuma zote zinazomhusu DC na kuahidi kuzifanyia kazi na hata katika matumizi mabaya ya fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya Mbuyuni na Mradi wa Maji Chang’ombe amekabidhi majina kwa Mkuu wa Polisi.

Pia aliwataka viongozi wa Serikali wilayani humo kuwatumikia wananchi na si kujinufaisha, kwa sababu hafumbii macho viongozi wa aina hiyo na aliwataka wananchi kufuata taratibu za kisheria ili kuondoa migogoro isiyo ya lazima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles