24.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 24, 2023

Contact us: [email protected]

Kangi Lugola atoa kauli nyingine sakata la ushoga

Na Mwandishi Wetu-Dodoma

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema kamwe vitendo vya ushoga haviruhusiwi na kila kiungo kilichoumbwa na Mungu katika mwili wa mwanadamu kina kazi yake na Serikali haitakubali vibadilishiwe matumizi.

Kauli hiyo aliitoa bungeni Dodoma jana baada ya Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Saidi Haji, kusema anashangaa Serikali kuwa na kauli laini kuhusu vitendo vya ushoga lengo likiwa ni kubembeleza misaada.

Akachangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa 2019/2020, Haji alisema na kuongeza: “Kabla ya kuanza kuchangia, naanza na utangulizi ambao ni muhimu kwa ninavyoona. Katika siku za karibuni kumezuka mjadala kuhusiana na ndoa za jinsia moja, tumesikia kauli za mawaziri akiwamo Kangi Lugola na Waziri wa Mambo ya Nje (Balozi Agustino Mahiga).

“Katika kauli zao inaonekana kuna mtego juu ya kukubaliana na jambo hili na kukinzana na jambo hili, naomba niwaambie, iwe ni mtego ama ni bahati mbaya, sisi Watanzania hatutaingia katika mtego wa ushoga, Tanzania hatutaki ushoga. Iwe mmetumwa ama ni mtego Watanzania hatutakubali kuingia katika ndoa za jinsia moja.

“Tanzania ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni muungano wa Serikali za Zanzibar na Tanganyika na Zanzibar asilimia 95 ni Waislamu, kwa vyovyote suala la ushoga hawatalikubali. Nawaambia nyoosheni maneno, nchi yetu hikubali ushoga na huo ndio msimamo wa Watanzania.

“Nadhani mmenielewa, naumia moyoni mwangu kuona nchi iliyostaarabika yenye utamaduni wetu wa asili, leo (jana) kuna baadhi ya watu wanasingizia misaada iwe ajenda ya kututoa sisi na kutupeleka katika ubaradhuri, haiwezekani.

“Hili jambo ni baya na Watanzania hawataki kabisa, naomba viongozi wetu mkae kimya kama hamuwezi, leo (jana) nimesikia hapa tuna mawe ya chuma kule Liganga, hivi kwanini tusitumie akili zetu na vitu alivyotupa Mungu hadi tunafikiria kulainisha maneno mara hatutawanyanyasa, hatutawafanya hivi, watanyanyaswa kwa sababu sheria yetu haikubali ushoga.”

Baada ya Haji kutoa kauli hiyo, aliomba Mwenyekiti wa kikao cha jana ambaye ni Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kutoa taarifa kwa mzungumzaji.

Akitoa taarifa yake, Lugola alisema: “Naomba nimpe taarifa Khatibu, kwamba Bunge hili kwa mfano tunapokuwa tumekaa kupitisha bajeti, huwa tunatenga fedha kwa matumizi mbalimbali kama maji, barabara, afya na nyinginezo.

“Lakini kuna wakati tunaweza kuzibadilishia matumizi fedha, labda za maji ziende kwenye barabara au za afya ziende kwenye maji, hawa mashoga anaowazungumzia ambao ni binadamu wenye viungo mbalimbali vya mwili, viungo ambavyo mashoga wanavitumia, vina kazi maalumu kwa mujibu wa uumbaji wa Mungu.

“Serikali yetu kamwe haitaruhusu mwanadamu yeyote kubadili matumizi ya kiungo ambacho kimekusudiwa kwa ajili ya kutolea haja, kitumike katika matumizi mengine ambayo Mungu hakuyakusudia.

“Kwa hiyo nimpe taarifa kwamba, Serikali inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, kwanza tuna sheria yetu ya kanuni ya adhabu ambayo inazuia kubadilisha matumizi ya kiungo cha binadamu.

“Kwa hiyo asiseme labda Serikali inajichanganya kwenye jambo hili, ni maelekezo ambayo tunatoa labda vyombo vinaripoti tofauti, lakini Serikali yetu kamwe, Tanzania ni hekalu la Roho Mtakatifu. Hatuwezi kukubali hekalu la Roho Mtakatifu likatumika kwa mambo ambayo hayakubaliki,” alisema Lugola.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,074FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles