27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Uhuru azima kiaina mjadala wa siasa 2022

NA ISIJI DOMINIC



KAULI ya Rais Uhuru Kenyatta kuelekea Uchaguzi Mkuu 2022 imezima mjadala kuhusu nani atakayemrithi lakini pia imetafsiriwa kumpa nafasi kutekeleza ahadi alizozitoa wakati wa kampeni.

Mara kadhaa Rais Uhuru amekuwa akiwataka wanasiasa kuacha kupiga siasa na badala yake kuwatumikia wananchi. Hata kitendo chake cha Machi 9, mwaka huu kuridhia kufanya kazi na kinara wa upinzani, Raila Odinga, kililenga kuwaleta pamoja wanasiasa ili kufanya kazi zitakazowanufaisha wananchi.

Mapema wiki iliyopita, wanasiasa kutoka Mkoa wa Kati ambako pia anatoka Rais Uhuru walikutana na kueleza masikitiko yao kutengwa na Rais hususani kuelekea Uchaguzi Mkuu 2022. Kuna kundi linataka Rais Uhuru kuanza kumpigia debe Naibu Rais William Ruto na lingine likitaka marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Katiba kurudisha nafasi ya Waziri Mkuu ambapo wanapendekeza Uhuru awanie.

Wale ambao wamekuwa wakitaka Rais Uhuru aendele kuwapo madarakani hususani kwa kurudisha cheo cha Waziri Mkuu wamekuwa wakisema umri wa Uhuru atakapokuwa anamaliza muhula wake wa pili ‘si afya kwa yeye kustaafu’. Wameenda mbali na kuhoji, hata akistaafu na umri mdogo atakuwa anafanya kazi gani?

Rais Uhuru akiwa ziarani Nyeri kufungua soko la Karatina, aliamua kuwajibu wanasiasa hao na inadaiwa kilichomkasirisha ni kitendo cha wabunge hao kutumia vyombo vya habari kueleza dukuduku lao badala ya kuonana naye. Pia alikasirishwa kwanini wanajadili siasa badala ya mambo ya msingi yanayogusa wananchi wa eneo lao.

Uhuru alivunja ukimya kuhusu mjadala ya mrithi wake akisisitiza chaguo lake litawashangaza wengi. Rais pia alisema atajihusisha kikamilifu na chochote kitakachotokea baada ya yeye kustaafu na kwamba ukimya wake kwa sasa usichukuliwe kama udhaifu.

“Wanafiriki kwa sababu Uhuru ataenda nyumbani 2022, hatakuwa na neno kuhusu nini kitakachotokea. Ninawaambia wakati muda mwafaka ukifika, nitakuwa na kitu cha kuongea,” alisema Rais Uhuru katika mkutano wa hadhara.

“Wengine wanafikiri nimenyamaza kwa sababu siwezi kuongea kuhusu siasa. Mimi bado ni mwanasiasa. Watashangaa chaguo langu muda huo utakapofika, lakini kwa sasa nataka nijihusishe na kutekeleza ahadi nilizotoa kwa Wakenya,”

Rais aliwaambia watu kutoka Mlima Kenya ambapo ni chimbuko lake lake la kuzaliwa kwamba atawashauri njia ya siasa ya kufuata muda sahihi ukifika na kueleza kukerwa na baadhi ya viongozi wanaotumia muda mwingi kupiga siasa badala ya kujishughulisha na miradi ya maendeleo.

Aidha Rais Uhuru alisema muda huo ukifika atawaambia wananchi ni viongozi gani hawapaswi kuchaguliwa kwa sababu muda mwingi waliutumia kupiga siasa. Kutokana na ushawishi alionao, wachambuzi wa siasa za Kenya wanasema kauli ya Rais huenda ikawabadili msimamo wanasiasa ambao wanashindwa kuwatumikia wapiga kura wao na kuamua kujadili siasa za 2022.

Rais Uhuru ambaye anahudumu muhula wake wa mwisho aliwashangaa viongozi wenye ajenda ya kutaka kumuona anaendelea kubaki madarakani.

“Kenya ilifanya uchaguzi mara mbili mwaka 2017, watu wamechoka na siasa za kila mara na wanachotaka ni maendeleo na kupata huduma,” alisema Rais alipokuwa Nyeri.

Wanasiasa ambao kutwa nzima wanapiga siasa tena ile ya nani atakayemrithi Rais Uhuru, nia yao ni kuvuruga zile ajenda nne kuu alizozitoa akiamini zitaboresha maisha ya wananchi.

Rais Uhuru pia aliweka wazi nia yake ya kustaafu muda wake wa kuongoza ukifika mwisho na kusema wale wanaotaka mabadiliko ya baadhi ya vipengele vya Katiba watahitaji kupata baraka ya wananchi ambayo anaamini yatalenga kuboresha maisha yao.

Ni dhahiri kundi kubwa la wanasiasa linataka Rais Uhuru kumtaja nani atakayevaa viatu vyake lakini wanasahau Rais ndiyo kwanza ametimiza mwaka moja wa muhula wake wa pili na lengo lake atakapoondoka madarakani ni kuona Kenya moja isiyo na doa ya ufisadi.

Hili linaweza likawa ngumu kutekeleza endapo ataruhusu naye kujihusisha kupiga siasa. Hata kukubali kufanya kazi na Raila kumetafsiriwa na baadhi ya wanasiasa kwamba anapanga kumtosa Naibu Rais Ruto na kumuunga mkono Raila endapo ataweka nia yake wazi ya kuwania urais 2022.

Rais Uhuru ametumia busara kuamua kufanya kazi na Raila na viongozi wengine wa upinzani kwa sababu anafahamu asingefanya hivyo, angepata wakati mgumu kutekeleza majukumu yake kutokana na ushawishi alionao Raila kwa wabunge wa NASA na wananchi.

Wakenya wameshuhudia hali ya utulivu kwa miezi ya hivi karibuni na wanataka uhusiano mzuri walioonesha Uhuru na Raila utumike kupambana na ufisadi na pia kupunguza gharama ya maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles